
Na Mwandishi wetu, Arusha.
Tanzania imeshuka katika viwango vya uhuru wa habari kwa mwaka 2025, hali ambayo imeelezwa kuwa inatokana na matukio mbalimbali yaliyojitokeza kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu.
Akizungumza jijini Arusha katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Aprili 29, 2026 Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Anna Henga amesema kushuka huko kunachangiwa na mazingira ya uchaguzi yaliyokuwa na changamoto kwa sekta ya habari.
Amesema matukio hayo yameathiri moja kwa moja utendaji wa waandishi wa habari pamoja na uhuru wa vyombo vya habari, hali iliyosababisha kupungua kwa kiwango cha uhuru huo nchini.
Aidha, amesema kuwa changamoto hizo zimejitokeza katika vipindi tofauti vya mchakato wa uchaguzi, kuanzia kabla ya kampeni, wakati wa upigaji kura, pamoja na kipindi cha baada ya uchaguzi.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari, Musa Juma amesema kuna umuhimu mkubwa kwa serikali kufanya maboresho ya haraka ya sheria zinazohusu wanahabari.
Amesema maboresho hayo yataondoa vikwazo vinavyokwamisha uhuru wa vyombo vya habari, pamoja na kulinda haki ya wananchi kupata taarifa sahihi na kwa wakati.
Aidha, amesisitiza kuwa uhuru wa habari ni msingi muhimu wa demokrasia, na kwamba bila uwepo wake sauti ya wananchi hupotea.
Social Plugin