Na Bora Mustafa - Arusha.
Akizungumza Leo Aprili 30,2026 jijini Arusha katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Mhe. Makonda amesisitiza kuwa taasisi zote za Serikali zinapaswa kufungua milango kwa wanahabari na kuacha tabia ya kuwazungusha wanapohitaji kupata taarifa mbalimbali.
Ameeleza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya taasisi au maafisa watakaobainika kukwamisha upatikanaji wa taarifa kwa vyombo vya habari, akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuimarisha uwazi na uhusiano mzuri kati ya Serikali na vyombo vya habari ili wananchi wapate taarifa sahihi na kwa wakati.
Aidha, amehimiza kuwepo kwa mfumo wa pamoja kati ya Wizara na wadau wa habari ili kuhakikisha maazimio yanayotolewa yanatekelezwa kwa vitendo badala ya kubaki kwenye majadiliano ya vikao pekee.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa madhimisho hayo, Bi. Asha Abinallah amesema maadhimisho hayo yaliandaliwa na kamati inayojumuisha takribani mashirika 20, yakiratibiwa kupitia Media Convergence.
Amesema kuanzia Aprili 28 hadi 30, wadau wa habari walikutana Jijini Arusha kujadili changamoto na mustakabali wa sekta ya habari nchini.
Bi. Asha alibainisha kuwa kupitia majadiliano hayo, wadau walipitisha maazimio 15 yaliyogawanywa katika makundi ya serikali, vyombo vya habari na wanahabari wenyewe.
Miongoni mwa maazimio hayo ni kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, kuboresha mazingira ya kiuchumi ya sekta, kuongeza uwazi wa upatikanaji wa taarifa, pamoja na kuweka miongozo ya matumizi salama ya teknolojia na akili Unde (AI) katika tasnia ya habari.
Picha : MAKONDA AONGOZA MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI... 'ACHENI KUTANGAZA WATU, TANGAZENI NCHI"

Social Plugin