Serikali imesema itaendelea kuratibu na kuimarisha Sera, Sheria na Miongozo inayosimamia programu za Mafunzo ya Uanagenzi na kuhamasisha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wanagenzi nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu amesema hayo leo Machi 03,2026 katika chuo cha ufundi stadi Daon Bosco jijini Dodoma wakati akifungua Awamu ya Nane ya Mafunzo ya Stadi za Kazi kwa Njia ya Uanagenzi kwa Vijana 5,746 waliodahiliwa katika Vyuo 46 nchini kwa mwaka 2025/26 ambapo utekelezaji wa programu umewezesha jumla ya wanufaika 93,495 hadi kufikia Februari, 2026.
Waziri Sangu amesema mafunzo hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuwapa vijana uzoefu wa kazi kwa nadharia na vitendo, kupunguza pengo la ujuzi kati ya mafunzo ya kitaaluma na mahitaji ya waajiri na kuongezeka kwa ajira kwa vijana kuajiriwa au kujiajiri.
“Hii ni dhamira ya dhati ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kujenga nguvukazi yenye ushindani na tija kwa maendeleo endelevu ya Taifa.” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania inahitaji nguvukazi yenye ujuzi, weledi na uwezo wa kutumia teknolojia ili kuhimili ushindani wa kikanda na kimataifa, huku Serikali ikiendelea kuboresha sera, sheria na mifumo ya mafunzo kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Awali akitoa salamu za wananchi wa Dodoma, Mkuu wa Mkoa huo Rosemary Senyamule ameipongeza serikali kwa kuendelea kutenga bajeti maalum kwa ajili ya mafunzo ya uanagenzi hatua ambayo inaonyesha wazi kuwa serikali inawekeza katika rasilimali muhimu za taifa hususani Vijana.
Kwa upande wake Naibu Katibu, Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Zuhura Yunus amesema Serikali kupitia Ofisi hiyo, inatekeleza Mafunzo ya Uanagenzi kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi Nchini kuanzia mwaka 2016/17 na dhumuni la programu hiyo ni kukuza ujuzi wa nguvukazi iliyopo katika soko la ajira ili kuongeza tija kwenye uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma.
Naye, Mkuu wa Chuo cha Don Bosco Dodoma, Mhandisi Dkt. Justine Mulebya, ameshukuru Serikali kwa kukipatia chuo hicho wanafunzi 650 na ameiomba kuwawezesha vifaa wahitimu wa mafunzo ya uanagenzi ili kuwawezesha kujiajiri na kuajiri vijana wengine wakihitimu mafunzo yao.







Social Plugin