Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA NA ALGERIA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA OLIMPIKI


Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai, alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Chama cha Kamati za Kitaifa za Olimpiki za Afrika (ANOCA), Bwa. Mustapha Berraf, tarehe 01 Machi, 2026, katika Ofisi za Michezo ya Vijana Afrika, jijini Algiers.

Kupitia mazungumzo hayo, wawili hao walijadili kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kwenye masuala ya olimpiki. Kadhalika, waliangazia namna ya kuimarisha ushirikiano wa michezo kwa ujumla kati ya Tanzania na Algeria kupitia Wizara za Michezo za nchi hizo mbili.

Viongozi hao, walisisitiza kwamba kukamilisha na kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) kwenye eneo la michezo, kutaimarisha ushirikiano huo. Mhe. Balozi Njalikai alisisitiza umuhimu wa kutoa kipaumbele kwenye eneo la mafunzo sambamba na kuandaa programu maalumu za mafunzo ya olimpiki kwa ajili ya vijana ili kuwajengea uwezo wa kushiriki na kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Kwa upande wake Bw. Berraf alionesha utayari wa kutoa kipaumbele maalumu kwa Tanzania kwenye eneo la mafunzo na kuahidi pia kuchagiza ukamilishwaji wa MoU kwenye eneo la michezo kati ya Tanzania na Algeria.

Mhe. Balozi Njalikai, alihitimisha mazungumzo yake kwa kumshukuru Bw. Berraf kwa kuonesha nia thabiti ya kuimarisha ushirikiano pamoja na juhudi anazofanya za kukuza vipaji vya vijana wa kitanzania kimichezo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com