Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imeendesha mafunzo maalum kwa walipakodi kuhusu Mfumo wa IDRAS (Integrated Domestic Revenue Administration System), mfumo mpya wa kielektroniki unaotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika usimamizi na ukusanyaji wa kodi za ndani nchini.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Bw. Emmanuel Maro, leo Jumanne Januari 27, 2026 katika ukumbi wa Makindo Hotel, yakilenga kuwaandaa walipakodi kabla ya kuanza rasmi kwa matumizi ya mfumo huo mnamo Februari 9, 2026.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Bw. Maro amesema kuwa mfumo wa IDRAS ni mfumo jumuishi wa kisasa unaounganisha huduma zote za usimamizi wa kodi za ndani katika jukwaa moja, kuanzia usajili wa mlipakodi, utozaji wa kodi, uwasilishaji wa matamko ya kodi, malipo, hadi ufuatiliaji na usimamizi wa taarifa za kikodi.
Ameeleza kuwa mfumo wa IDRAS unakuja kuchukua nafasi ya mifumo mbalimbali iliyokuwa ikitumika awali ndani ya TRA, huku ukiwa na lengo la kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya makaratasi (manual processes) na kuhamishia huduma zote za kodi kwenye mfumo wa kidijitali.
"Mfumo wa IDRAS umejengwa ili kurahisisha huduma kwa walipakodi, kuongeza uwazi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, sambamba na kupunguza makosa ya kibinadamu na mianya ya upotevu wa mapato", amesema Maro.Amefafanua kuwa kupitia mfumo huo, walipakodi wataweza kupata huduma mbalimbali ikiwemo usajili na uboreshaji wa taarifa za walipakodi, uwasilishaji wa matamko ya kodi (returns), makadirio na utozaji wa kodi, malipo ya kodi kwa njia za kielektroniki, ufuatiliaji wa madeni ya kodi, maombi ya marejesho ya kodi, mapingamizi ya maamuzi ya kikodi pamoja na maombi ya misamaha ya riba na adhabu.
Maro ameongeza kuwa mfumo wa IDRAS pia utawezesha utoaji wa huduma za leseni mbalimbali ikiwemo leseni za udereva, leseni za uzalishaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa pamoja na utoaji wa hati za ulipaji kodi (Tax Clearance) moja kwa moja kwa walipakodi wanaostahili.
"Mfumo wa IDRAS umejengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayomwezesha mtumiaji kuupata muda wote, saa 24 kwa siku na siku saba kwa wiki, popote alipo kupitia lango la mlipakodi (Taxpayer Portal), hatua inayotarajiwa kuokoa muda na kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara",amesema.Ameeleza kuwa mfumo huo pia utakuwa na uwezo wa kutoa vikumbusho kwa walipakodi kuhusu tarehe za uwasilishaji wa ritani na ulipaji wa kodi, hatua itakayopunguza uwezekano wa walipakodi kutozwa riba na adhabu kutokana na ucheleweshaji.
Katika kuhakikisha uwazi na uaminifu, mfumo wa IDRAS utawezesha uthibitishaji wa nyaraka za kodi kwa kutumia misimbo ya QR (QR Codes), pamoja na kuwawezesha walipakodi kuona historia na kumbukumbu zao zote za ulipaji kodi.
Aidha, mfumo huo umeunganishwa na mifumo mingine ya taasisi za umma na binafsi, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha mifumo ya taasisi mbalimbali inawasiliana ili kuboresha utoaji wa huduma. Katika siku zijazo, IDRAS unatarajiwa kuunganishwa na mifumo ya malipo ya walipakodi (billing systems), mifumo ya mishahara (payroll systems) na mifumo ya uhasibu.
Bw. Maro amewahimiza walipakodi kutumia ipasavyo kipindi cha mpito (Pre-Launch) kilichowekwa na TRA kabla ya kuanza rasmi kwa mfumo huo, ikiwemo kuhakiki taarifa zao, kupata nywila (passwords), na kuthibitisha au kuteua wawakilishi wao wa kikodi.
Pia amewakumbusha walipakodi kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kisheria, ikiwemo uwasilishaji wa ritani za makadirio ya kodi ya mapato kwa mwaka 2026, huku ikiwasihi kushirikiana na mamlaka hiyo ili kuhakikisha mafanikio ya utekelezaji wa mfumo mpya wa IDRAS.
Kwa upande wao, walipakodi walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za biashara zao na kutekeleza wajibu wao wa kikodi kwa hiari na kwa kuzingatia sheria.
TRA imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu mfumo wa IDRAS kupitia njia mbalimbali zikiwemo vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, tovuti ya TRA pamoja na mafunzo ya ana kwa ana na ya mtandaoni, ambayo baadhi yake yamewekwa katika akaunti ya YouTube ya TRA ili walipakodi waweze kuyafuatilia kwa wakati wowote.

































































































Social Plugin