Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC SIMANJIRO AIPONGEZA WORLD VISION, AITAKA JAMII KUSHIRIKIANA KULEA NA KULINDA WATOTO WENYE ULEMAVU



Na Bora Mustafa, Manyara .

 Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mwl. Faki Lulandala, ametoa shukrani kwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoshirikiana na serikali kwa nia njema, akilitaja shirika la World Vision kuwa miongoni mwa taasisi zinazotekeleza miradi yenye matokeo chanya kwa jamii.

Akizungumza Machi 25,2026 amesema kuwa World Vision imekuwa mfano bora wa kuigwa kutokana na kazi zake zinazoonekana wazi, huku akizitaka asasi nyingine kuongeza juhudi ili kuleta mabadiliko halisi kwa wananchi. Pia, amesisitiza umuhimu wa jamii kushiriki kikamilifu katika malezi na utunzaji wa watoto wenye ulemavu.

Aidha, Lulandala amesema kuwa kupinga unyanyasaji dhidi ya watoto wenye ulemavu si jukumu la serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi. 

Ameeleza kuwa serikali haiwezi kufika kila kaya kwa wakati mmoja, hivyo ushirikiano wa jamii unahitajika ili kuhakikisha watoto hao wanapata haki zao.

“Serikali inaposema itatoa huduma za kijamii, haimaanishi inaweza kufanya kila kitu peke yake, bali inahitaji ushirikiano na wadau mbalimbali,” amesema Lulandala.

Pia ametoa wito kwa familia ambazo zinapata watoto wenye ulemavu kujitokeza na kushirikiana na jamii pamoja na taasisi husika ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili watoto hao.

Amesisitiza kuwa watoto wenye ulemavu wanapaswa kupewa fursa sawa katika elimu na ajira kama watoto wengine.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Graciani Makota, amelipongeza shirika la World Vision kwa kujitolea kwake katika shughuli za maendeleo, akisema kazi wanazofanya zina mchango mkubwa kwa jamii.

Naye mwakilishi wa World Vision, Johnson Robson, amesema lengo la warsha hiyo ni kujadili changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu na kubuni njia bora za kuzitatua. Ameongeza kuwa warsha hiyo pia inalenga kujenga uelewa miongoni mwa wadau na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wa watoto wenye ulemavu, mwakilishi kutoka Shule ya Sekondari Emboreet, Sinyati Moines Mbapaya, amesema wanahitaji walimu wenye taaluma maalum, vifaa vya kujifunzia pamoja na msaada wa familia na jamii ili waweze kufikia ndoto zao.

Kwa  upande wa Mtaalamu wa Jinsia, Ulemavu na Ujumuishi wa Jamii, Godfrey Kisemba, utafiti uliofanyika Septemba na Oktoba 2025 umebaini kuwa idadi kubwa ya watoto wenye ulemavu bado hawapati fursa ya elimu. Utafiti huo ulihusisha kaya 12,948 katika vijiji 11 vya kata za Oljoro No. 5 na Naberera.

Amesema miongoni mwa watoto 488 waliobainika kuwa na ulemavu, ni asilimia 38.1 pekee waliowahi kuandikishwa shule, huku asilimia 61.9 hawajawahi kabisa kupata elimu. Sababu zilizotajwa ni pamoja na umbali wa shule, umaskini, unyanyapaa, ukosefu wa vifaa saidizi na miundombinu isiyojumuisha mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Kwa upande mwingine, Mratibu wa Mradi wa Naberera, Samwel Charles, amesema wamefanikiwa kutoa msaada wa viti mwendo kwa watoto 50 pamoja na kuwawezesha wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutambua dalili za awali za ulemavu.

Amesema pia wamekuwa wakishirikiana na viongozi wa dini na jamii kutoa elimu ili kuondoa imani potofu kuhusu watoto wenye ulemavu, pamoja na kuboresha miradi ya elimu, afya na maji katika maeneo husika.

Kwa ujumla, viongozi hao wamehimiza ushirikiano wa karibu kati ya serikali, mashirika na jamii ili kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata haki zao zote bila ubaguzi.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com