
Mwezeshaji wa Mafunzo ya Akili Unde (AI) katika uandishi wa habari na Uthibitishaji na Uhakiki wa Taarifa (Fact - Checking), Kadama Malunde akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari mkoa wa Geita.



Afisa Mnadhimu na Utawala wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Adam Maro, akisalimiana na Mwezeshaji wa Mafunzo ya Akili Unde (AI) katika uandishi wa habari na Uthibitishaji na Uhakiki wa Taarifa (Fact - Checking), Kadama Malunde

Waandishi wa habari mkoani Geita wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu matumizi ya Akili Unde (AI) katika uandishi wa habari pamoja na mbinu za uthibitishaji na uhakiki wa taarifa, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na changamoto ya kusambaa kwa taarifa potoshi (misinformation na disinformation).
Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi leo Machi 25, 2026 na Afisa Mnadhimu na Utawala wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Adam Maro, katika ukumbi wa Bwalo la Polisi Geita.
Mafunzo hayo yamewashirikisha waandishi wa habari zaidi ya 20 kutoka vyombo mbalimbali vya habari mkoani humo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, ACP Maro amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuwa na uelewa wa kina juu ya matumizi sahihi ya teknolojia ya AI pamoja na mbinu za uhakiki wa taarifa, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na ongezeko kubwa la taarifa potoshi.
“Waandishi wa habari mmekuwa nguzo muhimu katika kuifanya nchi kuwa salama. Nawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya. Kazi zenu nyingi zinaendana moja kwa moja na jukumu letu la kulinda usalama wa raia na mali zao. Mkipata ujuzi wa kutambua na kudhibiti habari potoshi, mtasaidia kuifanya jamii kuwa salama zaidi,” amesema ACP Maro.
Ameongeza kuwa, waandishi wa habari na Jeshi la Polisi wanashirikiana kwa karibu katika kukabiliana na hatari mbalimbali zinazoweza kuathiri jamii, hivyo mafunzo hayo yatawasaidia waandishi kuboresha namna yao ya kufikiri, kuchambua na kuripoti habari kwa weledi zaidi.
Aidha, ACP Maro amewashukuru waandishi wa habari kwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuhamasisha amani, utulivu na mshikamano wa jamii.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita kwa kushirikiana na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kupitia Mradi wa UKWELI KWANZA, yakilenga kuwajengea uwezo waandishi hao katika matumizi ya teknolojia za kisasa na mbinu bora za uhakiki wa taarifa.
Mafunzo hayo yamewezeshwa na Mwezeshaji Kadama Malunde, ambaye ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Malunde 1 Blog, mwenye uzoefu mkubwa katika masuala ya uhakiki wa taarifa (fact-checking) na matumizi ya Akili Unde (AI) katika uandishi wa habari.















Social Plugin