Na Mwandishi wetu,Dodoma.
Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini Benson Ndiege ameiagiza Bodi ya chama cha Wanaushirika wanaomiliki hisa za asilimia 51 za benki ya ushirika(UJE ) - kampuni ndani ya benki ya Ushirika kuhakikisha inajiimarisha kiutendaji, kifedha na kimkakati.
Amesema hatua hiyo itasiadia kulinda na kuendeleza umiliki wa asilimia 51 wa vyama vya ushirika ndani ya Benki ya Ushirika, akisisitiza kuwa UJE ni “jicho la Msajili ndani ya benki hiyo.”
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa ushirikiano unaoruhusu UJE kuanza kufanya kazi rasmi, Ndiege amesema uanzishwaji wa UJE ni matokeo ya dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufufua na kuimarisha sekta ya ushirika nchini, ikiwemo kuanzishwa kwa Benki ya Ushirika kama chombo cha kimkakati cha kuwawezesha wanaushirika kiuchumi.
Amesema kupitia msukumo wa Rais Samia, Serikali iliwezesha mtaji wa awali wa shilingi bilioni tano kwa wanaushirika, hatua iliyoongeza imani na uwezo wa vyama kuwekeza kwenye benki hiyo.
Katika maelekezo yake, Msajili ameitaka Bodi ya UJE kuitisha Mkutano Mkuu wa Wanachama wote kabla ya Machi 31, 2026, kwa lengo la kueleza wazi mikakati, maono na madhumuni ya kuanzishwa kwa UJE, pamoja na mwelekeo wa muda mrefu wa uwekezaji wao ndani ya benki.
Pia ameielekeza Bodi hiyo kuhakikisha inaweka mkakati madhubuti wa kuhamasisha vyama vya ushirika ambavyo bado havijawekeza kwenye benki kufanya hivyo, akisema uwekezaji wa asilimia 48 utabaki wazi ili kutoa fursa, elimu na hamasa ya kutosha kwa vyama zaidi kujiunga.
“UJE haiwezi kusimama bila mpango wa maono. Lazima ijipange mapema, itangaze nafasi za uongozi kwa uwazi, iandae vyanzo vya uhakika vya mapato na kuhakikisha benki inapata soko kupitia wanachama wake,” amesema Ndiege.
Ameongeza kuwa UJE inapaswa kuandaa na kuwasilisha taarifa za mara kwa mara kuhusu mwenendo wa benki, akisisitiza kuwa ofisi ya Msajili iko tayari kutoa usaidizi wowote wa kitaalamu unaohitajika.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Ushirika, Ng’ura Godfrey, alitambulisha rasmi Bodi ya UJE inayomilikiwa na vyama vya ushirika wenye hisa za asilimia 51, akisema hatua hiyo ni mwanzo wa ukurasa mpya wa kihistoria katika sekta ya ushirika nchini.
“Tunaandika historia, hatupaswi kurudia makosa ya nyuma. Hii ni taasisi ya wanaushirika. Tunataka ushirikiano huu uwe endelevu kadri mtaji unavyoongezeka,” amesema Godfrey, huku akiishukuru Bodi ya mpito ya UJE kwa ubunifu wake wa kuingiza bidhaa mpya sokoni katika kipindi cha mpito.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UJE, Profesa Gervas Machimu, amesema makubaliano hayo yanaweka msingi wa kuhakikisha benki inabaki mikononi mwa wanaushirika, akisisitiza wajibu wa wafanyabiashara na wanachama kulinda chombo hicho cha pamoja.
“Hatutaikwamisha benki. Tutahakikisha tunahamasisha wanaushirika kuendelea kuwekeza kwa misingi ya ushirikiano na kujali maslahi ya wengine,” amesema Prof. Machimu, akibainisha kuwa wanachama zaidi ya 1,540 tayari wamewekeza, huku wajumbe wote wa bodi wakitoka kwenye vyama vya ushirika.
Naye Mtendaji Mkuu wa UJE, Daria Rotu, amesema UJE inaanza kazi ikiwa na wanachama zaidi ya elfu moja, na itaweka mkazo katika kutambua mahitaji halisi ya vyama vinavyosimamiwa ili kushirikiana na benki kubuni huduma rafiki na zinazojibu mahitaji yao.
“Hatupo kinyonge. Tunajua vyama tunavyovisimamia na haki zao. Tutahakikisha vinapata huduma stahiki na fursa za uwekezaji,” amesema Rotu.

Social Plugin