Na Gideon Malima, Dodoma
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na VETA, imeendelea kufanya tafiti mbalimbali zinazolenga kuendeleza na kuboresha biashara ya senene katika mkoa wa Kagera.
Hayo yamebainishwa leo Januari 30,2026 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Mjini Mha. Johnston Mutasigwa aliyehoji, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wauza senene masoko na vifaa bora vya kutegea senene.
"Mpaka sasa, teknolojia rahisi ya mfano (prototype) itakayosaidia katika uvunaji wa senene imebuniwa na kutengenezwa,"amesema.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutafuta na kufungua masoko ya uhakika kwa bidhaa za senene.
"Hii inajumuisha kuwaunganisha wafanyabiashara wa senene na masoko ya miji mikubwa nchini, kuwashirikisha katika maonesho ya biashara ya kitaifa na kikanda, na kutangaza senene kama bidhaa ya kipekee ya Kanda ya Ziwa yenye uwezo wa kuingia kwenye masoko mapana ya Afrika Mashariki na kwingineko,"ameongeza.
Sambamba na hayo, akigusia suala la mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wa Senene, Mhe. Londo amesema Serikali kushirikiana na Manispaa ya Bukoba inaedeleza mradi wa ujenzi wa Soko la Senene katika sokomla Mjini unaoitwa Senene Complex.
"Lengo ni kuwaweka wafanyabiashara wote wa Senene pale na kutengeneza mazingira rafiki ambayo yatasaidia katika suala zima la Biashara ya Senene na kuhisiana suala la uwezeshwaji kupitia Serikali za Mitaa na kwakuwa sasa hivi tunaenda kwenye bajeti ni imani yangu kwamba suala hilo litaingizwa kama ombi maalum la juu ya bajeti ya 2026/27 na sisi kama Wizara ya Viwanda na Biashara tutashirikiana nao katika kuhakikisha kwamba Serikali inaweka msukumo kwenye hilo,"amesema.


Social Plugin