Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AJALI YA LORI LA MCHELE NA BASI LA KISIRE YAUA DEREVA, KUJERUHI ABIRIA 12 TINDE


Na Michael Abel - Shinyanga

Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea asubuhi ya leo Januari 27, 2026, katika eneo la Mnadani, Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
Ajali hiyo imehusisha basi la abiria la kampuni ya KISIRE lenye namba za usajili T 229 EEL, lililokuwa likitoka Kahama kuelekea Mwanza, kugongana uso kwa uso na lori la mizigo lililokuwa likibeba shehena ya mchele kutoka Dar es Salaam kwenda Rwanda lenye namba za usajili RAE 849N.


Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amesema aliyefariki ni dereva wa lori hilo, huku majeruhi 12 wakikimbizwa katika Hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.


Amesema kati ya majeruhi hao, 5 wapo katika hali mbaya na wanaendelea kupatiwa huduma za dharura chini ya uangalizi wa madaktari bingwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga huku wengine 7 wakipatiwa matibabu katika kituo cha afya Tinde.


Kamanda Magomi amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe na mwendokasi, unaodaiwa kufanywa na dereva wa lori alipokuwa akijaribu kulivuka gari lililokuwa mbele yake katika jaribio la kukwepa mkokoteni uliokuwa umebeba matikiti kuelekea mnadani, dereva huyo alishindwa kudhibiti lori na kugongana uso kwa uso na basi lililokuwa likitokea Kahama kuelekea Mwanza.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com