Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM CHAWAPANDISHA VYEO WANATAALUMA, YUMO DKT. DOTTO KUHENGA!

Dr. Dotto P. Kuhenga

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimetangaza kuwapandisha Vyeo Vya kitaaluma watumishi wake tarehe 20 Juni 2025, baada ya kupitia na kuidhinisha mapendekezo ya Kamati ya Ajira na hivyo Baraza la Chuo kuyapitisha. 

Kupitia taarifa iliyotolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Prof. Bonaventure Rutinwa, wahadhiri watatu wamepandishwa kutoka cheo cha Mhadhiri kwenda Mhadhiri Mwandamizi:

1. Dkt. Mamta T. Pandey (F) – Idara ya Sosholojia na Anthropolojia, Chuo cha Sayansi za Jamii (CoSS). Tangu alipopandishwa kuwa Mhadhiri mwezi Januari 2015, amepata jumla ya alama 5.00 kutoka kwenye machapisho na ufundishaji.

2. Dkt. Teresia E. Nkya (F) – Idara ya Microbiology/Immunology na Parasitology/Entomology, Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mbeya (MCHAS). Tangu apandishwe cheo Mei 2019, amepata alama 5.12 kutoka kwenye machapisho na ufundishaji.

3. Dkt. Dotto P. Kuhenga (M) – Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC). Tangu apandishwe kuwa Mhadhiri Julai 2020, amepata alama 5.00 kutoka kwenye machapisho na ufundishaji. Dkt. Kuhenga anakuwa mhadhiri mwandamizi wa kwanza katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma tangu Shule hiyo iwe sehemu ya Chuo Kikuu cha DSM.

Aidha, Baraza la Chuo kimeidhinisha pia kupandishwa kwa wahadhiri wengine kutoka ngazi ya Profesa Mshiriki kwenda Profesa Kamili:

1. Prof. Stephen O. Maluka (M) – Taasisi ya Masomo ya Maendeleo (IDS). Tangu apandishwe kuwa Profesa Mshiriki Oktoba 2019, amekusanya alama 9.20 (6.50 kutoka machapisho ya kisayansi, 0.70 kutoka ushauri elekezi na 2 kutoka ufundishaji).

2. Prof. Gastor C. Mapunda (M) – Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu, Chuo cha Binadamu (CoHU). Tangu apandishwe Januari 2019, amekusanya alama 10.07 (8.07 kutoka machapisho na 2 kutoka ufundishaji).

Kwa upande mwingine, Dkt. Elisante E. Mshiu (M) kutoka Idara ya Jiolojia, Shule ya Migodi na Jiolojia (SoMG), amepandishwa kutoka Mhadhiri Mwandamizi hadi Profesa Mshiriki. Ameshinda cheo hicho baada ya kukusanya alama 8.050, ikiwa ni pamoja na 5.287 kutoka machapisho ya kisayansi, 0.250 kutoka kitabu na makongamano, 0.513 kutoka ushauri elekezi, na 2 kutoka ufundishaji.

Chuo kimewapongeza wote waliopandishwa kwa juhudi na mchango wao katika kukuza taaluma, utafiti na ubora wa elimu ya juu nchini.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com