Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ODDO MWISHO : CCM RUVUMA HAITAMUANGUSHA RAIS SAMIA – YAJAYO YANAFURAHISHA



Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Ruvuma  Oddo Kilian Mwisho akizungumza na wananchi waliojitokeza katika tukio maalum la matembezi ya hisani ya Wanalizombe Marathon Mkoani Ruvuma katika uwanja wa majimaji Songea 

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma,  Oddo Mwisho, ambaye ndie  mgeni rasmi katika matembezi ya hisani ya Wanalizombe Marathon, amewahamasisha wananchi, hususan wanawake na vijana, kujitokeza kushiriki katika siasa na nafasi za uongozi. 

Matembezi hayo yamehudhuriwa na viongozi wa serikali na chama akiwemo Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngolo Malenya,na pia matembezi hayo yameandaliwa na Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Fro Events yakiwa yamebeba ujumbe wa “Umoja, Amani, Ushiriki wa Vijana na Wanawake katika Uongozi wa Kijamii kwa Demokrasia.”

Akizungumza katika kilele cha matembezi hayo,  Mwisho amewapongeza waandaaji na washiriki wa matembezi hayo kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha mshikamano. 

Amesema tukio hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha jamii kuhusu uchaguzi wa amani, kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uongozi na kuenzi historia ya mashujaa wa Majimaji kutoka Songea. 

Amesisitiza kuwa wanawake wa Ruvuma wanapaswa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, kwani ni haki yao ya msingi.

Kwa niaba ya wana-Ruvuma,  Mwisho amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa utekelezaji madhubuti wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi. 

Ametaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni upatikanaji wa maji safi na salama, upanuzi wa miundombinu ya barabara, usambazaji wa umeme vijijini, maendeleo ya sekta ya afya na elimu pamoja na kuimarika kwa sekta ya kilimo kupitia ruzuku ya pembejeo na dawa.

Akigusia maendeleo ya kimkakati, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia imedhamiria kukuza uchumi wa Mkoa wa Ruvuma kupitia ujenzi wa reli ya kisasa ya Mtwara–Mbambabay–Mchuchuma–Liganga kutoka Ludewa 

Aidha, amebainisha kuwa ujenzi wa bandari ya Mtwara na Mbambabay unaendelea kwa kasi, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 80 zimeelekezwa kwenye utekelezaji wake. 

Barabara kuu zimewekwa lami na miundombinu mingine imeboreshwa kwa kiwango cha hali ya juu.

Kwa upande wa usafiri wa anga, Mwenyekiti wa UWT Mkoa Sarah Mgoli amewasilisha maombi kwa niaba ya wanawake wa Ruvuma kutaka kuongezwa kwa ruti za ndege hadi Songea, ili kuwawezesha wananchi kufanikisha majukumu yao kwa wakati. 

 Mwisho ameunga mkono hoja hiyo, akiitaja kuwa ni ishara ya maendeleo ya haraka yanayohitajika mkoani humo.

Mwisho  amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama na serikali na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao. 

Amesisitiza kuwa CCM Ruvuma iko imara na haitamuangusha Rais Dkt. Samia wala chama cha taifa. 

Amemaliza  kwa kusema, “Yajayo yanafurahisha,” akiwataka wananchi kuwa na amani, mshikamano na matumaini kwa maendeleo zaidi.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com