
Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Takribani viongozi zaidi ya 4,000 wa ngazi ya mashina katika Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, wamepatiwa mafunzo ya kisheria kwa kipindi cha siku tatu kuanzia tarehe 10 Mei 2025.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Kanisa la Anglikana Songea Mjini na yamehusisha mabalozi wa nyumba kumi, wajumbe wa mashina pamoja na watendaji wake.
Lengo la mafunzo hayo ni pamoja na kutoa elimu ya utawala bora, uraia, mbinu mbadala za utatuzi wa migogoro, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia pamoja na elimu ya uchaguzi.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, ameambatana na timu nzima ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (Samia Legal Aid).

Aidha, Mhe. Ndumbaro ameeleza kuwa msaada wa kisheria uliotolewa kwa wananchi wa Songea ni sehemu ya shukrani kwa ukarimu mkubwa waliouonesha kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake ya Tamasha la Sanaa na Utamaduni Mkoani Ruvuma.
Amesema kuwa ziara hiyo siyo tu imeleta heshima kwa mkoa huo, bali pia imechochea Serikali kuendelea kusogeza huduma mbalimbali kwa wananchi zikiwemo barabara, vituo vya afya na huduma za elimu.
Katika kuhitimisha Waziri Ndumbaro ametoa wito kwa wananchi wote waliojiandikisha kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa kupiga kura, akisisitiza kuwa hiyo ni njia mojawapo ya kulinda na kudumisha demokrasia na maendeleo ya taifa.
Amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika jamii.


Social Plugin