RAIS SAMIA AELEZA ANAVYOISIKIA SAUTI YA MAGUFULI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinumwi Adesina kushoto, wakiondoa kitambaa kuashiria uwekaji wa Jiwe la Msingi mradi wa Ujenzi wa Barabara ya mzunguko wa nje katika mji wa Dodoma itakayotoka Ihumwa-Matumbulu-Nala-Veyula-Ihumwa Kilometa 112.3 Hafla hiyo imefanyika kwenye Sherehe zilizofanyika leo tarehe 09 Februari, 2022 katika eneo la Veyula Jijini Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wananchi katika Sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi Ujenzi wa Barabara ya mzunguko wa nje katika mji wa Dodoma itakayotoka Ihumwa-Matumbulu-Nala-Veyula-Ihumwa Kilometa 112.3 katika Sherehe zilizofanyika katika eneo la Veyula Jijini Dodoma.

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog-DODOMA.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma yenye urefu wa Kilomita 112.3 huku akieleza namna anavyoisikia sauti ya mtangulizi wake hayati Dkt.John Magufuli akimtaka kuendeleza miradi mingine yote aliyoiacha .

Rais Samia amesema atahakikisha anaiendeleza miradi yote iliyoachwa na Dk. John Pombe Magufuli na kuwataka wananchi kuitunza.

Kauli hiyo ameitoa leo Februari 9,2022 wakati akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa arabara ya mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma( km 112.3).

Rais Samia amesema siku ya leo toka asubuhi anasikia sauti ya mtangulizi wake ikimueleza kuhusu miradi aiyoiacha ikiwemo ya kuhamia Dodoma na mingine ikiwemo huu wa barabara ya mzunguko wa nje Dodoma.

"Ndugu zangu siku kama ya leo mimi mwenzenu toka asubuhi nasikia sauti ya mtangulizi wangu Dkt John Pombe Magufuli ananiambia kuhusu miradi hii ,,kuhusu Dodoma kuwa makao makuu, kuhusu mambo mengi.

Na leo hii tupo hapa kuweka jiwe la msingi la mradi huu lakini kàzi hii waswahili wanasema ukiona vinaelea vimeundwa na kwa bahati nzuri muundaji wa suala hili aliyetekeleza maono ya taifa kuhamia Dodoma akataka kuipanga Dodoma ,kwa bahati mbaya hatunaye,Mungu amemchukua,

Lakini ameniachia urithi mzito nami niahidi mawazo yote aliyoyaanzisha nita kwenda kuyatekeleza kikamilifu,leo hii ni moja kati ya mawazo aliyoyaanzisha niahidi pamoja na kuungwa mkono na African Bank tunaenda kukamilisha mradi huu kama alivyotaka Magufuli,"alisisitiza Rais Samia.


Katika hatua nyingine Rais huyo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema Serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi wa barabara ambapo gharama ya ujenzi wa kilomita 1 ni shilingi bilioni 1.2 hadi 1.5 hivyo amewaomba watanzania kuzitunza.


Amesema ujenzi wa barabara hiyo unaenda kufungua masoko hivyo ametaka ujenzi huo ukamilike kwa wakati kwani utatoa fursa mbalimbali hivyo watanzania kujiongezea kipato.


"Ndugu zangu Benki kudhamini miradi 11 hii inadhihirisha kweli hii ni Benki kwa ajili ya Waafrika,"amesema.


Amesema kilomita moja ni shilingi bilioni 1.2 hadi 5 hivyo amesema Serikali inatumia fedha nyingi hivyo kutumia nafasi hiyo kuwaomba watanzania Kutunza Miundombinu na kuacha mambo ya hovyo yanayofanywa katika uharibifu huo.


Kadhalika Rais Samia amesema Serikali inajenga barabara 23 kwa fedha za ndani huku 13 kazi ikiwa inaendelea.



"Tunashukuru sana Serikali ya awamu ya tano kuleta vuguvugu hili pamoja na kuungwa mkono na Benk ya Maendeleo na hawapo katika barabara wapo pia katika maji na umeme tumewaomba kutusaidia katika uwekezaji wa watu,"amesema


Akiwasilisha taarifa ya Mradi huo,Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Rogatus Mativila amesema lengo la kujenga barabara hiyo ni kupunguza msongamano katika Jiji la Dodoma.

Amesema jumla ya gharama ya Mradi huo ni shilingi bilioni 249 ambazo ni Kwa ajili ya fidia na ujenzi ambapo amedai kuna miradi midogo midogo kama ujenzi wa vituo vya afya,ununuzi wa ambulance wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Mtendaji huyo wa TANROADS ameeleza kuwa lengo ni kupunguza msongomana mkubwa wa magari katika Mkoa wa Dodoma ambao ungesababishwa na muingiliano wa magari yanayosafiri kupitia mjini.

Ameeleza kuwa barabara hiyo ina umbali wa Kil 20 kutoka katikati ya Jiji la dodoma ikiwa imegawanywa kwa wakandarasi wawili ambao ni M/sAVIC INTL Project na China Civil Engineering Construction Cooperation zote kutoka Jamhuri ya watu wa China.

Alifafanua kuwa awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa Kilomita 52.3 kupitia Nala,Veyula,Mtumba na Ihumwa wakati awamu ya pili itahusisha Kilomita 60 kupitia Ihumwa, Matumbulu na Nala.

Kwa upande wake,Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika(AFDB) Dk. Akinwumi Adesina amesema wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ambapo amedai wanaamini Tanzania ni sehemu sahihi ya uwekezaji.

Amesema Benki hiyo imewekeza kwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali yenye thamani ya Dola za kimarekani bilioni 2.5.

"Miaka kadhaa iliyopita nilikaa na kuzungumza na rafiki yangu,mtu wa watu hayati Dk.Magufuli kuhusu kutekeleza mradi huu ,Kwa bahati mbaya hayupo tena lakini Kutokana na ushirikiano wake kwetu tunaahidi kuendelea kishirikina na watanzania kwa miradi mingi zaidi,"amesema.

Naye,Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali iliona kuna umuhimu wa Kujenga barabara hiyo kutokana na ongezeko la watu pamoja na Dodoma kuwa Makao Makuu hivyo magari yanayoingia na kutoka kuwa mengi.

"Tunatoa shukrani kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kutekeleza mradi huu,imetoa fedha nyingi katika miradi ikiwa ni pamoja na kulipa madeni ya wakandarasi,

Bila kuwa na Mahusiano mazuri hili lisingetokea niipongeze Wizara kwa mradi huu mkubwa ni ubunifu mkubwa na utafungua fursa nyingi hivyo ,"amefafanua.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments