RAIS SAMIA KUWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA UJENZI BARABARA YA MZUNGUKO WA NJE

 

Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 Blog-DODOMA.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.  Samia Suluhu Hassan kesho (Februari 9,2022) anatarajiwa kuweka jiwe la msingi  la mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje (Outer Ring Road) katika Jiji la Dodoma yenye urefu wa  Kilomita 112.3.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka ameeleza hayo mapema leo Februari 8,2022 Ofisini kwake jijini hapa katika kikao chake na waandishi wa habari na kuongeza kuwa barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami hali itakayoruhusu uwepo wa fursa mbalimbali.


Amesema hafla ya uwekaji jiwe la msingi itafanyika katika eneo la Makutupora-Veyula  kuanzia saa 1:00 asubuhi ambapo maandalizi yote muhimu yamekamilika.


Mkuu huyo wa mkoa wa Dodoma amefafanua kuwa ujenzi huo utagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania Bilioni 221 na kwamba ujenzi huo utakamilika ifikapo mwaka 2025 na kuweka mandhari safi ya Jiji la Dodoma.


Akitaja fursa zitakazo tokana na barabara hiyo,Mtaka amesema itakuwa kiungo muhimu kwa barabara nyingine za Jiji la Dodoma ikiwa imegawanywa Kwa wakandarasi wawili ambao ni M/sAVIC INTL Project  na China Civil Engineering Construction Cooperation zote kutoka Jamhuri ya watu wa China.


Mtaka pia ametumia nafasi hiyo kuzitaka taasisi zote za Serikali mkoani hapa,taasisi binafsi,makundi mbalimbali na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi katika hafla hiyo ili kubaini mapema fursa nyingi zitakazo patikana kupitia ujenzi huo.


Kwa kuwa wananchi Wana fursa nzuri ya kushiriki,Mtaka amelielekeza jeshi la polisi Mkoa wa Dodoma kuruhusu madereva wa  daladala (kukatisha ruti) kufanya usafirishaji wa abiria kutoka sehemu mbalimbali ili kurahisisha huduma hiyo ili watu waweze kufika kwa wakati katika eneo hilo.


Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa barabara nchini(TANROADS)Mkoa wa Dodoma Injinia Leonard Chimagu amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ya mzunguko utajengwa kwa awamu mbili .


Amefafanua kuwa awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa Kilomita 52.3 kupitia Nala,Veyula,Mtumba na Ihumwa wakati awamu ya pili itahusisha Kilomita 60 kupitia Ihumwa, Matumbulu na Nala.


Injinia Chimagu amesema ujenzi huo ukikamilika utafungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Dodoma ikiwa ni pamoja na kuondoa msongamano wa magari uliopo sasa kwa kuwa magari yanayoenda mikoa mingine watatumia  barabara hizo bila kupitia ndani ya Jiji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments