NBS YATOA HALI YA MFUMUKO WA BEI KUPUNGUA

 Mkurugenzi wa Sensa ya watu na Takwimu za Jamii (NBS)Ruth Minja

*****

Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog-DODOMA


OFISI ya Taifa ya Takwimu imesema mfumuko wa bei wa taifa unaoishia  Mwezi Januari 2022 umepungua hadi asilimia 4.0 kutoka asilimia 4.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba 2021.


Mkurugenzi wa Sensa ya watu na Takwimu za Jamii,Ruth Minja ameeleza hayo jana Jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu fahirisi za bei za Taifa kwa mwezi Januari mwaka huu .


Alisema kupungua huko kunamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Januari mwaka huu imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba 2021.


"Kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Januari mwaka huu kumechangiwa hasa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Januari mwaka huu ikilinganishwa na kipindi cha mwaka ulioishia Desemba 2021,"alisema


Licha ya hayo aliongeza kuwa mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Januari mwaka huu umepungua hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3.9 ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba 2021 .


"Mfumuko wa bei ambao haujumuishi vyakula visivyochakatwa,nishati na bili za maji(core inflation)kwa mwezi Januari mwaka huu umepungua pia hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 4.6 ilivyokuwa mwezi Desemba,2021,"alisema Minja.


Alitaja baadhi ya bidhaa zingine zisizo za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Januari mwaka huu ikilinganishwa  na mwaka ulioishia mwezi Desemba 2021 ni pamoja na mavazi kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia 2.8,viatu kutoka asilimia 4.6 hadi asilimia 4.4 na kodi ya pango kutoka asilimia 4.4 hadi asilimia 1.5.


Nyingine ni cherehani kutoka asilimia 9.1 hadi asilimia 5.0,simu janja kutoka asilimia 3.5 hadi 3.3,vyombo vya nyumbani kama sahani kutoka asilimia 16.7 hadi asilimia 3.6,luninga kutoka asilimia 3.5 hadi asilimia 1.2 na malazi kwenye hoteli na nyumba za kulala wageni kutoka asilimia 6.6 hadi asilimia 2.9.


MFUMUKO WA BEI KWA BAADHI YA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI.


Kuhusu hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki,Mkurugenzi wa Sensa ya watu na Takwimu  za  Jamii alieleza kuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Januari mwaka huu kwa Nchi ya Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Januari 2022 umepungua hadi kufikia asilimia 2.7 kutoka asilimia 2.9 Kwa mwaka ulioishia Disemba 2021.


"Kwa upande wa Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Januari mwaka huu umepungua hadi asilimia 5.39 kutoka asilimia 5.73 kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba 2021,"alifafanua .Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments