RPC MASEJO AFUNGUA MAFUNZO YA MWEZI MMOJA KWA ASKARI POLISI ARUSHA KUBORESHA UTOAJI HUDUMA BORA NA USALAMA WA WATALII


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP  Justine Masejo, akifungua mafunzo ya mwezi mmoja yanayohusisha Askari Polisi 15 kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Arusha 

Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha 

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP  Justine Masejo, amefungua mafunzo ya mwezi mmoja yanayohusisha Askari Polisi 15 kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Arusha yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino kampasi ya Arusha lengo likiwa ni kuboresha utoaji wa huduma bora pamoja na usalama wa watalii.

Akifungua mafunzo hayo leo Oktoba 20,2021 Kamanda Masejo amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linaunga mkono mkakati wa kuutangaza utalii duniani kupitia "Royal Tour" iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Askari wanafundishwa mambo mbalimbali lengo likiwa ni kuwa na askari wenye weledi na  utaalamu ambao watahudumia watalii vizuri  na kuhakikisha usalama wao.

Hali kadhalika ametoa shukrani kwa Chama cha Waendesha Shughuli za Utalii Tanzania (TATO) kwa kufadhili mafunzo hayo ambayo yatawajengea uwezo askari katika utendaji kazi ambapo amewataka kutumia fursa hiyo waliyoipata vizuri.

Naye Mkuu wa Idara ya utalii wa chuo hicho Bwana Ebenezer Goroi amesema katika mafunzo hayo Askari watapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo namna bora ya kuhudumia watalii, tamaduni mbalimbali za watalii, jinsi ya kukabiliana na msongo wa mawazo, ulinzi na usalama wa watalii, kutatua matatizo mbalimbali ya watalii na majukumu ya Jeshi la Polisi katika kutoa huduma kwa watalii.

Ufunguzi huo umehudhuriwa na Katibu Mtendaji wa TATO Bwana Siriri Akko, Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma Bwana Vicent Baraka, Wahadhiri wa Chuo hicho ambao wamesema mafunzo hayo yataongeza ufanisi kwa Jeshi la Polisi hususani katika utoaji wa huduma bora kwa watalii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments