MTAKA AWAZUIA WAKUU WA IDARA,MADIWANI KWENDA MBEYA KUJIFUNZA... AONYA WATUMISHI KUTUMIA LUGHA ZA HOVYO

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka (kulia) akisikiliza kero za watumishi wakati wa kikao kazi baina yake na watumishi wa Serikali Jijini Dodoma.

**

Na Dotto Kwilasa, Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amezuia ziara ya Wakuu wa Idara na Madiwani wa Jiji la Dodoma kuidhinishiwa fedha kiasi cha Shilingi milioni 47 kwa ajili ya kwenda Mbeya kujifunza namna ya uendeshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumzia leo katika kikao na watumishi wa Jiji la Dodoma,Mkuu huyo wa Mkoa alisema Madiwani 55 waliomba waidhinishiwe bajeti ya shilingi milioni 26,watumishi 14 shilingi milioni 7.6,usafiri wa kukodi Shilingi milioni 6 na mafuta Shilingi 5.7.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema Madiwani na Wakuu hao wa Idara walimwandikia barua ya kuomba fedha hizo kwa lengo la kwenda kujifunza masuala ya usafi wa mazingira ,ukusanyaji wa mapato na namna ya kutokomeza ziro mashuleni jambo ambalo amesema linatia shaka.

Amesema,Wakuu hao wa Idara pamoja na madiwani hawakupaswa kufanya hivyo kwani mambo wanayotaka kuyafuata Mbeya yapo Jijini Dodoma na kwamba fedha wanazohitaji zina thamani kubwa kiasi cha kujenga madarasa ya kisasa mawili.

"Hivi kweli uchukue hela za madarasa mawili kwa ajili ya ziara ya kujifunza kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako na unaishi nacho,Dodoma Kuna miradi mingapi ya kujifunza,hapa kuna utekelezaji wa miradi mingi unaendelea shida ni uvivu wa kufikiria na si vinginevyo,"amesema.

Amesema kitendo hicho ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali ambazo zinatokana na kodi za Wananchi masikini huku akiongeza kuwa katika maelekezo ya Ofisi yake, Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma inapaswa kujitafakari Kuhusu jambao hilo.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma ametahadharisha watumishi wa Jiji hilo kuacha matumizi ya lugha za hovyo wanapowahudumia Wananchi na kusema kuwa hali hiyo inakwamisha juhudi za Serikali katika kumaliza migogoro iliyopo.

Akiongea katika kikao hicho Mtaka amesema kuwa ili mambo yaende lazima watumishi hao wawe na lugha nzuri kwa wanao wahudumia.

Amesema,migogoro mingi ikiwemo ya ardhi inaibuka Kila kukicha Kutokana na changamoto ya mahusiano mabaya baina ya ofisi nyingi za serikaki na Wananchi hivyo kuwataka kuona haja ya kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma.

"Mnakuwa na lugha chafu za hovyo,mnawaudhi wananchi mpaka wanaogopa kufuata huduma maofisini kwenu,hamna kabisaa huduma nzuri kwa watu mnaowahudumia,mnakwamisha maendeo,"amesema Mtaka.

Licha ya hayo ameeleza kuna wakati wananchi wanaonekana kama kero lakini kikwazo kikubwa ni watumishi wenyewe ndiyo tatizo .

"Kuna kipindi tulichukua jukumu la utatuzi wa migogoro ya ardhi tuliamini ufumbuzi wake umefikia mwisho,lakini hali badi ipo palepale,wapumzisheni Wananchi wanaotumia muda mwingi kutafuta suluhu za changamoto zao huku shughuli zao za uchumi zinalala,"alisema.

Mbali na hayo amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri kufanya ubunifu kuona haja ya kusikikiza kero za Wananchi kwa kujadiliana kwa uhuru ili kumaliza migogoro .

"Hapa mjadala wetu tunafanya ili kumaliza kero za Wananchi wa Dodoma, ,kunguru mwoga huepusha ubawa wake kika mmoja abaki kwenye nafasi yake,
wekeni utamaduni wa kuelezana ukweli,"amesema.

Kikao hicho kimehusisha watumishi kutoa Idara mbalimbali wakiwemo idara ya fedha,watumishi wa Ofisi ya ukaguzi na uchaguzi,watumishi wa Kitengo cha nyuki,Idara ya kilimo,biashara na Maendeleo ya jamii.
Baadhi ya watumishi wa Jiji la Dodoma wakisikiliza kwa makini maelekezo ya mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka katika kikao kazi kilichowakutanisha watumishi wa idara mbalimbali.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments