70% YA WATOTO CHINI YA MIAKA 5 HAWANYONYESHWI IPASAVYO


Mama akimnyonyesha mwanae huku akili na mawazo yake yote yakiwa kwa huyo mwanae kuonesha upendo na kumjali
Ofisa Lishe mkoa wa Singida Teda Sinde akifafanua jambo kuhusiana na suala zima la Unyonyeshaji 
Mtoto akifurahia ziwa pamoja na mapenzi ya karibu ya mama yake
**

Na Abby Nkungu, Singida

ZAIDI ya asilimia 70 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano
 mkoani Singida, huwa hawanyonyeshwi maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya, hali inayoathiri afya zao, malezi, makuzi na usalama wa kundi hilo katika jamii.

Takwimu kutoka Idara ya lishe mkoa wa Singida zimekuja wakati huu ambapo Dunia inaadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji maziwa ya Mama ili kulinda afya na kuimarisha kinga ya watoto.

Utafiti wa Kitaifa wa mwaka 2018/19 juu ya Hali ya lishe mkoani
Singida, unaonesha asilimia 27.9 ya watoto wa chini ya miaka mitano
ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya na asilimia 3 tu ya watoto walio na umri wa chini ya miaka miwili ndio angalau hupata mlo unaokubalika katika tafsiri ya lishe bora.

"Hii ndio sababu kubwa ya watoto wengi kuwa na matatizo ya lishe na kiafya ambapo hali halisi inaonesha asilimia 29.8 ya watoto walio
chini ya miaka mitano wana udumavu, asilimia 5 ukondefu na asilimia 15 wana uzito mdogo",alisema Ofisa Lishe mkoa wa Singida, Teda Sinde.

Alisema kuwa matatizo hayo yametokana na familia nyingi kuacha
kuzingatia suala la Uzazi wa Mpango; hivyo kujikuta wakizaa mtoto
mwingine kabla ya yule wa awali kutimiza miaka miwili.

Alieleza kuwa jambo hilo husababisha mtoto wa awali kuachishwa
 kunyonya, hivyo kuathiri afya, malezi, makuzi, usalama na matunzo kwa mtoto aliyetangulia kwa kuwa mzazi au mlezi hulazimika kuhamishia mapenzi kwa mtoto mchanga aliyezaliwa.

Dk. Suleiman Muttani ambaye ni Daktari Bingwa mshauri wa magonjwa ya wanawake na watoto katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida, alieleza kuwa mtoto kutonyonyeshwa maziwa ya mama kwa miaka isiyopungua miwili kama inavyoshauriwa, hupata athari mbaya za kiafya.

"Baadhi ya athari hizo ni pamoja na ukuaji duni wa ubongo hivyo kusababisha mtoto kutofundishika kirahisi na kuwa mzito kwenye kufikiria na kutoa maamuzi, husababisha upungufu wa damu mwilini, huathiri mfumo wa kinga ya mwili kwa ajili ya kupambana na magonjwa na kupata utapiamlo na magonjwa mengine ambayo yanaweza kusababisha vifo", alisema.

Hata hivyo, baadhi ya akinamama; akiwemo Agatha Majoya na Nyagili Soteri wanasema kuwa tatizo kubwa ni elimu duni juu ya umuhimu wa Uzazi wa Mpango huku Hamoud Hafidh na Ali Alute wakidai kuwa imani potofu juu ya baadhi ya njia kuwa na madhara ya kiafya, ni changamoto nyingine.

Mwito wao ni kwa Waatalamu wa afya, maofisa lishe na wadau wengine kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa Uzazi wa mpango na kukemea mila potofu ili kuhakikisha kila mtoto anapata kikamilifu haki ya maziwa ya mama kama inavyoshauriwa na Wataalam wa afya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post