DKT. KALEMANI APIGA MARUFUKU UPANDISHAJI WA BEI YA GESI NCHINI | MALUNDE 1 BLOG

Thursday, August 19, 2021

DKT. KALEMANI APIGA MARUFUKU UPANDISHAJI WA BEI YA GESI NCHINI

  Malunde       Thursday, August 19, 2021


 Hafsa Omar-Dodoma
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewapiga marufuku wauzaji na wasambazaji wa Gesi za majumbani kupandisha bei ya bidhaa hiyo.

Amepiga marufuku hiyo Agosti 18, 2021, Jijini Dodoma alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye maduka mbalimbali kwa wauzaji wa gesi hiyo.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, Serikali haitakubali kuona wafanyabiashara wanajipangia bei kubwa ambazo zinawaumiza Watanzania.

“Ninawapa onyo la mwisho wafanyabiashara wote wa gesi za majumbani kutopandisha bei, pia Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) walishatoa maelekezo, Mimi Waziri wa Nishati napita sasa kutoa onyo la mwisho, tukirejea wakati mwingine na kukuta bei imepanda tutachukua hatua ikiwa ni pamoja na kukufungia biashara husika kwa mtuhumiwa”, alisisitiza Dkt.Kalemani.

Alifafanua kuwa, Mtungi wa ujazo wa kilo 6 unatakiwa kuuzwa kati ya shilingi 20, 000  hadi  shilingi 21,000 na Mtungi wa ujazo wa kilo 15 unauzwa kati ya shilingi 47,000 hadi shilingi 50,000 na bei hiyo ni kwa wauzaji wa jumla na rejareja.

Aidha, alisema kuwa Serikali inafahamu bei ya gesi katika soko la dunia imepanda lakini si kwa kiasi kikubwa ambacho inawafanya wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa hiyo hata kuliko namna ilivyopanda katika soko la dunia.

“Serikali inaendelea kufuatilia bei ya Soko la dunia na kama bei itapanda sana mtaelekezwa na kupewa utaraibu na EWURA lakini kwasasa haitapanda hatutaki kuleta kero kwa wananchi alisema”, alisema Dkt. Kalemani.

Hata hivyo, aliwataka wafanyabiashara hao endapo watapata changamoto yoyote wawasiliane na EWURA ili waweze kupewa utaratibu unaotakiwa.

Pia, aliwaagiza Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuchukua hatua kali kwa yoyote ambae atakiuka maagizo hayo.


Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post