ZIMAMOTO YATOA TAMKO UUNGUAJI WA SHULE NCHINI

Na Mwandishi Wetu
JESHI la Zimamoto na Uokoaji nchini limewataka wamiliki wa shule nchini kuhakikisha wanafunga vifaa maalumu vya awali vya kuzimia moto ili kuweza kudhibiti majanga pindi yanapotokea na kupunguza athari za majanga hayo

Hayo yalisemwa na Kaimu Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, DCF Charo Mangare baada ya kutembelea Shule ya Msingi ya Byamungu Islamic iliyopo Kata ya Itera, wilayani Kyerwa mkoa wa Kagera ambapo kulitokea ajali ya moto na kusababisha vifo vya wanafunzi 10 na majeruhi sita.

“Pamoja na kuwaagiza wamiliki wa shule kufunga vifaa maalumu vya kudhibiti moto pia nawaagiza makamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini kukagua shule zote na zoezi hilo liwe endelevu ili kuweza kudhibiti madhara ya ajali hizo pindi zinapotokea” alisema DCF Mangare

Akizungumzia chanzo cha ajali hiyo DCF Mangare alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama inaendelea na uchunguzi na pindi utakapokamilika taarifa itatolewa kwa wananchi ili kuwepo sasa mbinu za kudhibiti ajali kama hizo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Muuguzi Mkuu Msaidizi, Justine Katalaiya alisema majeruhi wanne kati ya sita waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya Karagwe wamehamishiwa Hospitali ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post