MKUU WA MKOA AHAMASISHA WATU 'KUPIGA NYUNGU' ...DC AOMBA VIONGOZI WANAOJIFUKIZA WATUPIE PICHA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa wito kwa wananchi na wadau wote mkoani humo kuhakikisha wanachukua hatua za tahadhari ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa Afya pamoja na kushauri matumizi ya Nyungu kwa ajili ya kujifukiza.

Amehamasisha hayo ikiwa ni katika kuunga mkono kauli ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na viongozi wengine wa juu nchini katika kupambana na Covid – 19 ambao huenezwa kwa kuingiwa na majimaji yatokayo kwa njia ya hewa wakati mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya au kugusa majimaji yanayotoka puani mwa mtu aliyeathirika.

“Nitoe wito kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na nyini waheshimiwa madiwani kuchukua hatua za tahadhari ya ugonjwa huu kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wetu wa afya. Tukumbuke kuwa virusi vya Corona ni janga la kidunia na linaua, Aidha matumizi ya Nyungu kwa ajili ya kujifukizia yanashauriwa na Mh. Jafo waziri wa OR-TAMISEMI pamoja na viongozi wengine wa juu tuyazingatie, watu wapige Nyungu,” Alisisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi ambaye pia anakaimu Wilaya ya Sumbawanga Mh. Said Mtanda akifafanua michanganyiko ya aina tatu inayoshauriwa na wataalamu wa tiba ya asili yaliyofanyiwa majaribio na kituo cha Tiba asili kinachotambulika na serikali amesema moja ya mchanganyiko ni kutumia mti wa mwarobaini, tangawizi iliyopondwa, majani ya mpera, limao zilizokatwa  unachemsha pamoja na kisha kujifunika na kuvuta moshi kwa pua na mdomo ili moshi huo uingie mwilini na hatimaye kwenda kuua virusi vya Corona.

“Sisi kule Namanyere (Wilayani Nkasi) tumeweka utaratibu wa kuhamasishana kujifukiza, kwa sababu ukiona aibu matatizo kweli utayapata, kwa hiyo kiongozi ukiwa unajifukiza unakapiga kapicha kidogo unawatumia wengine ili waseme hee hata Diwani kajifukiza, kwa hiyo wale unaowaongoza watahamasiska kujifukiza kwa sababu wataona kumbe sasa hili sio suala la aibu,” Alisema.

Viongozi hao wamesema hayo wakati wa vikao vya madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na Wilaya ya Sumbawanga katika vikao vya Mabaraza ya Madiwani ya Halmashauri hizo kuhusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post