NAIBU WAZIRI WA AFYA DKT. NDUGULILE ATAKA TAARIFA UTOAJI WA DAWA HOSPITALI YA RUFAA IRINGA

Na Mwandishi Wetu Iringa

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amemuagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Atupele Mwandiga kuhakikisha anapata taarifa ya utoaji wa dawa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa.

Agizo hilo limekuja mara baada ya ziara ya yake mkoani humo alipotembelea hospitali hiyo kujionea utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kushuhudia mmoja wa mama aliyejifungua Hospitalini hapo kupewa dawa mara moja badala ya mara tatu kama iilivyoandikwa na Daktari.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa amekasirishwa na utendaji kazi wa manesi katika wodi ya Mama na Mtoto kwa kutozingatia utoaji huduma hasa kuhakikisha wazazi na watoto wanapewa dawa kwa wakati zinazotakiwa na kwa idadi sahihi.

Ameongeza kuwa lengo la mgonjwa kupewa huduma ni kuhakikisha anapona na sio kufanya aendelee kupata tabu na shida hivyo Serikali ya Awamu ya Tano imewekeza fedha nyingi katika kuhakikisha Sekta ya Afya inaboreshwa nchini.

"Haiwezekani mgonjwa kanunua dawa zake kwa fedha zake lakini bado hata hamzingatii kumpatia dawa mnategemea ataponaje” alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha Dkt. Ndugulile ameutaka uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kuhakikisha wanaratibu utoaji wa huduma hospitalini hapo ili kuepukana na malalamiko ya wagonjwa na kupoteza imani ya wananchi kwa Hospitali hiyo.

"Tukiendelea hivi tutaondoa imani kwa wananchi wetu katika utoaji wa huduma za afya sisi tunatakiwa kutoa huduma kwa wananchi na sio kuwapa kero wananchi" alisema Dkt. Ndugulile.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Atupele Mwandiga amemuahikikishia Naibu Waziri Dkt. Ndugulile kusimamia utoaji huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na kusimamia vilivyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma inayostahili.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya tano imetoa kiasi cha Billioni 7 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya na maboresho katika Zahanati na vituo vya Afya mkoani humo katika kuhakikisha inaboresha Sekta ya Afya hivyo watasimamia Sekta hiyo kikamilifu.

"Mhe. Naibu Waziri tutahakikisha hatutopoteza imani ya wananchi katika utoaji huduma za afya na tutatendea haki rasimali fedha tulizopewa na Serikali katika kuboresha Sekta ya Afya Mkoani kwetu" alisema Dkt. Atupele

Wakati huo huo Dkt. Ndugulile ametembelea na kujionea utendaji kazi utoaji wa huduma kwa wananchi katika Ofisi ya Bima ya Afya (NHIF), Kampeni ya masuala ya Lishe, Kiwanda cha Ruaha Milling na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile yuko katika ziara ya siku mbili mkoani Iringa kukuagua shughuli za Afya na Maendeleo ya Jamii mkoani humo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post