MAZUNGUMZO KATI YA DPP NA KIGOGO TAKUKURU YAKWAMA


Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania, Kulthum Mansoor amedai wameshindwa kufikia muafaka wa makubaliano baina yake na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Wakili wa utetezi Elia Mwingira, alitoa madai hayo jana kwamba awali walimwandikia DPP barua ya kuomba kukiri makosa yanayomkabili mshtakiwa, lakini mazungumzo yamevunjika.

Alitoa madai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Isaya.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake bado haujakamilika.

Wakili wa utetezi Mwingira, alidai kuwa kwa kuwa mazungumzo na DPP yamevunjika upande wa Jamhuri uharakishe upelelezi.

Wakili Wankyo alidai wataelekeza wapelelezi kuhakikisha wanakamilisha upelelezi katika maeneo yaliyobaki.

Hakimu Isaya alisema mshtakiwa ataendelea kukaa mahabusu na kesi hiyo itatajwa Januari 20, mwaka huu.

Mansoor anakabiliwa na mashtaka manane ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha Sh. bilioni 1.477.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527