BOMU LILILOTEGWA NDANI YA GARI LAWAUA WATU ZAIDI YA 40

Zaidi ya watu 40 wamedaiwa kuangamia kwenye mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari Mogadishu nchini Somalia.


Bomu hilo imeripotiwa lilipuka wakati wa pilka pilka nyingi asubuhi katika kituo kimoja cha kukagua magari eneo la makutano ya barabara jijini Mogadishu.

Walioshuhudia mlipuko wa bomu hilo wanasema kwamba idadi ya waliofariki dunia huenda ikaongezeka.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Habari la BBC, walioshuhudia wamedai mlipuko huo ulikuwa mbaya zaidi.

Kufikia sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo lakini kwa kipindi kirefu wapiganaji wa kundi la al-Shabab wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara katika taifa hilo.


Tangu mwaka 2007 kundi la kigaidi la Al-Shabab limekuwa likifanya juu chini kuipindua serikali kuu ya Somalia.

Mwaka 2011, Al Shabab lilifurushwa kutoka mji mkuu Mogadishu kwa ushirikiano wa jeshi la Somalia na vikosi vya Umoja wa Afrika vilivyotumwa nchini humo AMISOM; hata hivyo hadi sasa kundi hilo la kigaidi lingali linashikilia baadhi ya  maeneo ya vijijini nchini humo

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na katika miaka ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wa kundi la al-Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post