DAKTARI KIZIMBANI KWA UHUJUMU UCHUMI, KUTOA MIMBA


Daktari wa Hospitali ya Dental Clinic, Awadhi Juma (40) na mwenzake, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwamo na ya utoaji wa mimba. Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni muuguzi wa hospitali hiyo, Kidawa Ramadhani (26).


Washtakiwa hao kwa pamoja walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, akisaidiana na Wakili wa Serikali Glory Mwenda, kwa nyakati tofauti waliwasomea washtakiwa hao mashtaka yao.

Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa kuwa Oktoba, mwaka huu, eneo la Sinza Mori, jijini Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa na lengo la kutoa mimba, waliingiza bomba la sindano katika sehemu za siri za wanawake wawili tofauti (majina yamehifadhiwa) na kusababisha kuharibika kwa mimba zao.

Ilidaiwa kuwa Agosti, 2002 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Juma kwa lengo la kudanganya, alighushi cheti cha Diploma cha Utaalamu wa Tiba ya Kinywa akionyesha ni halali kimetolewa na Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi za Afya Muhimbili wakati akijua si kweli.

Mshtakiwa Juma pia anadaiwa kwamba Februari 20, 2015 jijini Dar es Salaam, alighushi leseni ya biashara ya tarehe hiyo akionesha imetolewa na Manispaa ya Kinondoni wakati akijua si kweli.

Ilidaiwa kwamba kati ya Mei, 2015 hadi Desemba 4, mwaka huu, mshtakiwa huyo alikutwa akimiliki hospitali ya tiba ya meno bila kibali.

Ilidaiwa kwamba katika tarehe hizo, mshtakiwa huyo kwa nia ya kudanganya, alijiita daktari kinyume cha sheria huku akijua si kweli.

Katika shtaka jingine ilidaiwa kuwa katika tarehe za tukio la sita, Juma alitakatisha na kujipatia Sh. 260,000 wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa la jinai la kughushi.

Upande wa Jamhuri ulidai, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kesi iliahirishwa hadi Januari 10, 2020 kwa ajili ya kutajwa. Washtakiwa walirudishwa rumande kwa kuwa mashtaka ya kutakatisha fedha hayana dhamana.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527