Bashe: Wadau Zalisheni Mbegu Za Mazao Kwa Wingi

Serikali imewataka wazalishaji mbegu za mazao nchini kuongeza uzalishaji na ubora ili nchi iepukane na utegemezi toka nje.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa mbegu leo (Jumanne 24.09.2019) jijini Dodoma,Naibu Waziri wa Kilimo Husein Bashe amesema ili Tanzania ifikie malengo ya kukuza  uzalishaji wenye tija katika kilimo lazima ijitegemee kwa mbegu.

Amebainisha kuwa usalama wa chakula unategemea sana uwezo wa nchi kuzalisha mbegu za mazao ndani na si kutegemea wahisani.

 “Kuwa na nchi inayotegemea mbegu za mazao toka  nje kunaondoa dhana ya uhuru na kujitegemea,hivyo kuhatarisha usalama wa chakula na taifa” alisisitiza Naibu Waziri Bashe

Bashe amewaeleza wadau hao  kuwa Wizara ya Kilimo ina lengo la kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa mbegu hususan zinazozalishwa nchini.

Ameziagiza Taasisi za Utafiti wa Kilimo(TARI), Kampuni ya Mbegu (ASA) kushirikiana na wadau binafsi kuwekeza mitaji ili kuinua uzalishaji wa mbegu bora ili kukidhi  mahitaji ya wakulima.

“Ni budi sasa taasisi zetu za TARI na ASA zikaanza kuzalisha mbegu mara tatu kwa mwaka kwenye mashamba kwa njia  ya umwagiliaji badala ya kutegemea mvua “ Naibu Waziri alisema

Bashe amebainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina utegemezi wa mbegu asilimia 60 kutoka nje ya nchi.

Hali hiyo imesababisha mbegu nyingi kuuzwa kwa bei kubwa na zingine kulalamikiwa na wakulima kuwa na ubora mdogo.

Naibu Waziri Bashe amewataka wadau kutengeneza mpango maalum wa kuongeza uzalishaji kwani serikali pekee haiwezi kutokana na soko la mbegu kuwa kubwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao ,Wizara ya Kilimo  Nyasebwa Chimagu amesema kikao hicho kitajadili kwa mapana changamoto za upatikanaji mbegu bora na mfumo mzuri wa usambazaji mbegu nchini.

Nyasebwa aliongeza kusema kwa sasa wakulima wana malalamiko mengi  kuhusu upungufu wa mbegu ,hivyo wizara na wadau wana jukumu la kutafuta majawabu mapema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments