NAIBU WAZIRI BASHE ATUA WIZARANI, WAZIRI WA KILIMO AGAWA MAJUKUMU

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 22 Julai 2019 ameongoza kikao kazi cha uongozi wa juu wa Wizara ya Kilimo ili kutoa taswira ya muelekeo wa Wizara hiyo.


Kikao hicho kilichotuama kwa masaa kadhaa katika Ofisi ndogo za Wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam na kuongozwa na Mhe Hasunga, kimehudhuriwa pia Naibu Maziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) na Mhe Hussein Bashe kadhalika katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Mathew Mtigumwe.

Katika kikao hicho Waziri Hasunga amewataka Naibu Mawaziri hao kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili kutimiza adhma ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli akiwa na muktadha wa kuimarisha uchumi wa wananchi kadhalika maendeleo kwa ujumla wake.

Waziri wa Kilimo Mhe Hasunga ametoa taswira ya muelekeo wa wizara hiyo katika mipango ya muda mfupi na muda mrefu ili kuwa na weledi na utendaji uliotukuka katika utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/2020.

Rais Magufuli amemteua Naibu waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe akishika nafasi ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa ambaye sasa ni waziri wa Viwanda na Biashara.

Moja ya mambo aliyoyabainisha Mhe Hasunga ni pamoja na haja ya kuanzishwa kwa Sheria ya Kilimo itakayotoa suluhisho la changamoto zinazamkabili Mkulima na Sekta hiyo kwa ujumla.

“Kuna kila sababu ya kuanzishwa haraka sheria ya kilimo na tayari tupo katika hatua za mwisho, kwa sababu hatuna Sheria ya Kilimo na inayotumika sasa ni Sera ya Kilimo, iliyotungwa mwaka 2013 ambayo pia inahitaji kupitiwa upya” amesema

Mhe. Hasunga ameongeza kuwa Sheria zinazotumika kwa sasa ni za Bodi za Mazao mbalimbali, ambazo pia zinachangamoto zake na kuna mazao ambayo hayana Bodi kiasi kwamba kuwatetea Wakulima wa mazao hayo inakuwa vigumu.

Mazao yaliyo katika utaratibu wa Bodi ni pamoja na zao la Pamba, Kahawa, Chai, Korosho, Pareto na Tumbaku kwa upande wa mazao ya biashara, mazao ambayo hayana bodi ni yale ya chakula ambayo nayo yana mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa.

Kadhalika ameeleza kuhusu usajili wa wakulima wa mazao yote na ambapo Bodi hizo ziliagizwa kuwapatia vitambulisho kwa ajili ya kuwatambua wakulima hao na wanapofanyika kazi zao ili iwe rahisi kuwahuduma.

Pamoja na mambo mengine Mhe Hasunga ametaja umuhimu wa Wizara ya Kilimo kuanzisha Bima ya Mazao itakayokuwa suluhisho kwa wakulima nchini ambao kwa muda mrefu wamekosa utetezi pindi wanapopatwa na majanga kutokana na uchache wa mvua ama vinginevyo, jambo linalopelekea kukoseka kwa mazao ya kutosha.

MWISHO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527