WAZIRI BITEKO AZINDUA BODI YA BODI YA TAASISI YA JIOLOJIA NA UTAFITI WA MADINI TANZANIA (GST)

Asteria Muhozya na Samwel Mtuwa, Dodoma

Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), imetakiwa kuiwezesha taasisi hiyo kurahisisha maisha ya Wachimbaji Wadogo, wa Kati na Wakubwa kwa kuhakikisha wanapata taarifa za tafiti zinazofanywa na taasisi hiyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akizundua Bodi ya GST na kueleza kuwa, shughuli za utafiti ni moja ya maeneo muhimu katika sekta ya madini kutokana na kutoa uhakika kwa wachimbaji na hivyo kukidhi matarajio ya wadau.

Pia, ameitaka bodi kuiwezesha taasisi hiyo kutoa ubunifu mpya utakaowezesha taasisi hiyo kuongeza mapato kwa serikali kutokana na shughuli na huduma zinazotolewa na GST.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko ameitaka bodi hiyo kuhakikisha GST inapata Ithibati ya maabara yake ikiwemo kutangaza huduma zinazotolewa na maabara hiyo ili kuwawezesha wadau kuifahamu na kuitumia.

Aidha, ameitaka bodi husika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sera, sheria na taratibu zilizowekwa na kueleza kwamba, taasisi hiyo inao watendaji wazuri wa kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kiamilifu na kutumia fursa hiyo kumpongeza Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST Yokberth Myumbilwa, kwa kusimamia vema utendaji wa GST.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema taasisi hiyo ni kitovu cha sekta ya madini nchini na kwamba ndiyo imeshikilia mstakabali wa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa.

Ameongeza kuwa, bado yapo majukumu ya taasisi hiyo ambayo hayajafanikiwa na hivyo kuitaka bodi hiyo chini ya Prof. Ikungula kuhakikisha yanafanikiwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Justinian Ikingura amesema bodi hiyo inatambua umuhimu wa rasilimali madini katika kuchangia pato na kukuza uchumi wa taifa ikiwemo kutambua nia na lengo la Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.

Amesema ili kufikia lengo hilo, ni muhimu GST ikawezeshwa ipasavyo kupitia wizara ili iongeze kasi na tija zaidi katika kutekeleza majukumu yake, hususan katika maeneo ya kufanya utafiti na kukusanya taarifa muhimu za kijiosayansi za kubaini maeneo yenye miamba yenye vishiria vyakuwepo madini ya kimkakati yanayohitajika zaidi katika matumizi ya teknolojia ya viwanda vya kielekitroniki, zana za utafiti wa mawasala ya anga na matumizi maalum katika viwanda vingine, ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchini katika maeneo hayo. 

“Kwa mfano madini lithium, cobalt na palladium yanazidi kupata umuhimu wa pekee katika matumizi ya viwanda vya kimkakati. Hivi majuzi takriba wiki moja iliyopita bei ya Palladium ilifikia kiasi cha dola za kimarekani 1,600 kwa wakia na kuzidi hata dhahabu ambayo ikiwa karibu dola 1,300 kwa wakia moja. Lakini si wengi wanatambua madini ya Palladium ambayo yako katika kundi la metali za Platinum, yaani Platinum Group Metals (PGM),” amesisitiza Prof. Ikingura.

Ameongeza kuwa, eneo jingine ni uboreshaji wa huduma za maabara za uchunguzi na upimaji wa miamba na madini yake ili zikidhi viwango vya kimataifa, na hivyo kuvutia wawekezaji katika sekta ya madini kutumia zaidi maabara za ndani ya nchini badala ya kupeleka sampuli katika maabara za nje ya nchi, na hivyo kupoteza fedha za kigeni.

Vilevile, amesema ipo haja ya kuboresha na kuongeza thamani taarifa za jiofikizia na jiokemia zilizo katika hifadhi au kanzidata ya GST ili ziweze kuwa na thamani kubwa zaidi  kwa taifa na kwa wawekezaji katika sekta ya madini, suala ambalo  litaiweesha GST kuongeza maduhuli ya serikali kupitia wizara.

Mbali ya Mwenyekiti, wajumbe wa bodi hiyo ni Abdulkarim Hamisi Mruma, Emanuel Mpawe Tutuba, Bibi Bertha Ricky Sambo, Shukrani Manya, David R. Mulabwa na Bibi Monica Otaru.

Bodi hiyo imezinduliwa Machi 27, 2019 Makao Makuu ya GST, jijini Dodoma.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post