SERIKALI YAMWAGA MAGARI 26 KWA MAAFISA ELIMU MIKOA YOTE 26 TANZANIA BARA

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Katika kukabiliana na changamoto ya Usafiri  kwa maofisa elimu mikoa,Serikali  kupitia TAMISEMI imenunua takribani magari 26  kwa ajili ya  Maofisa elimu mikoa  katika mikoa yote  26 Tanzania bara.

Hayo yamesemwa  Machi 27 jioni , jijini Dodoma na Waziri wa  TAMISEMI Seleman         Jafo wakati akifunga mkutano mkuu  wa 6 wa maafisa elimu wilaya na mikoa Tanzania bara[REDEOA] ambapo amesema kuwa magari hayo yatarahisisha usafiri kwa maafisa hao katika kutembelea shule mbalimbali katika mikoa yao na kuibua changamoto na kuzifanyia ufumbuzi.

Mhe.Jafo amesema  huwa hapendi suala la uzembe katika ufuatiliaji hivyo amemwagiza katibu mkuu  wizara  ya TAMISEMI  ndani ya siku tisini magari hayo yawe yameshapatikana na kukabidhiwa kwa maafisa elimu wa mikoa.

Waziri Jafo amewataka Maafisa Elimu,Kujituma ,kujitoa na kuzipenda kazi zao huku akiwataka kuwaheshimu na kuwahurumia  watu wa chini yao wakiwamo walimu  na kuacha dhana ya kuwadharau  na badala yake kuwatia moyo ili wafundishe kwa kujituma.

Aidha ,Waziri Jafo amebainisha kuwa wizara  yake  hadi kufikia sasa imeshatenga  fedha  zaidi ya Tsh.Bil.18 kwa ajili ya vifaa vya maabara kwa shule 1200 hapa nchini.

Katika hatua nyingine Waziri huyo wa TAMISEMI amezungumzia juu ya suala la nidhamu ambapo amebainisha katika kizazi hiki kuna baadhi ya walimu wamekuwa wakivaa mlegezo wakiwa wanafundisha .

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Maafisa Elimu wilaya na mikoa Tanzania bara , [REDEOA] Bi.Germana Mung’aho  ambaye ni afisa elimu kutoka mkoani Mtwara amesema mambo  yote waliyojadili watayachanganua huku akiwashukuru wajumbe wote kwa kushiriki mkutano huo muhimu.

Mkutano mkuu  wa Maafisa elimu wilaya na mikoa Tanzania
bara[REDEOA]Umekutanisha maafisa elimu mikoa na wilaya kutoka mikoa yote 26 Tanzania bara na kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa ni Elimu bora itatufikisha  katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527