MAWAKILI SITA WAPITISHWA KUMRITHI FATUMA KARUME TLS


Mawakili sita wamepitishwa kugombea urais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) unaotarajiwa kufanyika Aprili mwaka huu kuchukua nafasi itakayoachwa wazi na Fatma Karume anayeshikilia nafasi hiyo.

Taarifa iliyotolewa jana na kamati ya uchaguzi wa TLS na kuthibitishwa na mtendaji mkuu wa chama hicho, Kaleb Gamaya imewataja wagombea hao kuwa ni mkurugenzi wa chama cha wanasheria watetezi wa mazingira (Leat), Dk Rugemeleza Nshala na aliyewahi kuwa Rais wa chama hicho, John Seka.

Wengine ni Godfrey Wasonga, Gaspar Mwanalyeka, Godwin Ngwilimi na Charles Tumaini.

Awali, Fatma alieleza nia yake ya kugombea tena nafasi hiyo lakini baadaye alibadili nia hiyo,

Uchaguzi wa TLS umekuwa ukivuta hisia kali, tangu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alipowania na hatimaye kushinda nafasi hiyo Machi 2017. Hata hivyo, Lissu aliitumikia nafasi hiyo kwa miezi sita tu baada ya kushambuliwa kwa risasi jijini Dodoma Septemba 7, 2017.
Na  Elias Msuya, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post