SALAMU ZA POLE KUFUATIA AJALI ILIYOUA WATU 19 SONGWE

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus E. Mwangela anatoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa ndugu, jamaa na marafiki wa wafiwa, kufuatia ajali ya gari iliyosababisha vifo 19 ikiwa wanaume ni 15 na wanawake wanne.

Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema kutokana na ajali hiyo iliyotokea usiku eneo la Senjele Wilayani Mbozi ikihusisha magari matatu yaliyokuwa yakielekea Mbeya kugongana, serikali Mkoani Songwe imetoa majeneza 19 pamoja na usafiri kwa ajili ya kuhifadhi miili ya marehemu.

“Rais Magufuli amenituma niwape pole na ametuelekeza kama Mkoa kusimamia Mamlaka za Usalama barabarani kufanya uchunguzi na hatua zinazo stahili kuchukuliwa, pia ameelekeza tujipange vizuri kukabiliana na matukio ya ajali za barabarani”, amesema Brig. Jen. (Mst) Mwangela.

Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema chanzo cha ajali hiyo kimetokana na gari la abiria aina ya coaster kugongwa na gari la mizigo lililokuwa nyuma yake kisha coaster kugonga gari la mizigo lililo kuwa mbele yake na kupelekea gari la abiria kubanwa katikati ya magari mawili ya mizigo.

Aidha ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, kuweka utaratibu maalumu wa magari kupita kwa kupokezana katika maeneo yote yenye miteremko mikali, kuwepo ukaguzi wa magari kabla hayajaanza kushuka au kupanda mlima pamoja na kuweka ulinzi wa maeneo hayo.

“Mungu ametupa akili za kufanya kazi na akili hizi tuzitumie kuzuia ajali ndani ya Mkoa wa Songwe, hivyo nawasihi watumiaji wote wa vyombo vya moto kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani ili kuweza kuepuka ajali kama hizi”, amesisitiza Brig. Jen. (Mst) Mwangela.

Mapema jana Brig. Jen. (Mst) Mwangela amefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songwe ambapo miili ya marehemu ilikuwa imehifadhiwa ili kuwafariji wafiwa waliofika kutambua miili ya ndugu zao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post