MBOWE,MATIKO KUENDELEA KUSOTA MAHABUSU HADI JANUARI 17..MAWAKILI WAHOJI KWA NINI?


Wakati Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko wakiendelea kusota mahabusu, Wakili anayewatetea Profesa Abdallah Safari amehoji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuhusu rufaa iliyokatwa na upande wa mashtaka katika Mahakama ya Rufani.

Mbowe na Matiko wanasota mahabusu baada ya Mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana yao Novemba 26,2018 kwa kukiuka masharti ya dhamana, ambapo waliamua kukata rufaa Mahakama Kuu lakini iliwekewa pingamizi baada ya upande wa mashtaka kukata rufaa Mahakama ya Rufani.

Profesa Safari alihoji swali moja kuhusu rufaa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi kueleza kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa.

Profesa Safari alimuuliza Wakili Kadushi kama rufaa waliyoikata ilikuwa chini ya hati ya dharura na kama hawakufanya hivyo ni kwa nini...? 

Katika majibu yake Wakili Kadushi ameeleza kuwa hakuna uhalali wa kisheria kuhusu swali hilo mahakamani hapo, labda lingeulizwa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufaa.

Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi January 17, 2019 huku akisema swali hilo la rufaa wakalihoji Mahakama Kuu.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 112/ 2018 ni wabunge wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), John Mnyika (Kibamba), John Heche (Tarime Vijijini), Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda Mjini).

Pia wamo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018 maeneo ya Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post