WATOTO WAWILI WAFARIKI WAKIOGELEA BAHARINI KUSHEREHEKEA MWAKA MPYA

Watu wawili ambao ni wanafunzi wa shule ya Msingi Mgao Mkoa wa Mtwara wameokotwa wakiwa wamefariki dunia pembezoni mwa mwambao wa Bahari ya Hindi.

Uchunguzi wa Daktari imebainisha kuwa vifo hivyo vimetokana na kukosa hewa baada ya kuzama kwenye maji.

Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Blasius Chatanda amesema tukio la wanafunzi hao kuzama majini limetokea Januari Mosi katika kijiji cha Mgao ambapo uchunguzi wa awali unaonyesha watoto hao hawakuwa na wasimamizi walipokwenda kuogelea.

"Watoto hao tumeweza kuwatambua, wa kwanza alikuwa anaitwa Rajab Athman mwenye umri wa miaka 12 ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne, wa pili alikuwa anaitwa Salum Hamza ambaye alikuwa na miaka 8. Walikwenda kuogelea kwenye fukwe na bahati mbaya maji yaliwazidi na wakapoteza maisha," amesema Kamanda Chatanda.

Katika hatua nyingine siku hiyo ya Januari Mosi Amri Nayope ambae ni mwanafunzi wa shule ya Sekondari alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitari ya Wilaya ya Newala akidaiwa kushambuliwa kwa kupigwa na watu ambao hawakufahamika kisha kutelekezwa jirani na nyumbani kwao.

Kufuatia taarifa hiyo baadhi ya wakazi mkoani hapa wameitaka jamii hususani wazazi na walezi kuongeza umakini katika kuwasimamia watoto wao.

Kamanda Chatanda amesema msako mkali unaendelea kuwabaini waliohusika katika shambulio lililopelekea kifo cha mwanafunzi huyo wa sekondari huku miili ya wanafunzi wa shule za msingi tayari imesha kabidhiwa kwa ndugu baada ya uchunguzi wa Daktari ili kuendelea na taratibu za mazishi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post