RAIS MAGUFULI AMPOTEZEA SPIKA NDUGAI OMBI LA MAWAZIRI KUCHOKA WAPEWE LIKIZO


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amewaombea likizo mawaziri na manaibu waziri kwa Rais John Magufuli. 


Spika Ndugai ametoa maombi hayo kwa Rais Magufuli wakati akitoa salamu katika hafla ya uapisho wa viongozi wa serikali iliyofanyika leo tarehe 9 Januari 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

“Nikiwaangalia mawaziri nawaona mmechoka hivi mnakwenda likizo kweli?, ninawaombea kwa rais likizo hata ya mara moja kwa mwezi,” amesema na kuongeza Spika Ndugai.

“Mawaziri wetu wamekuwa wakifanya kazi kubwa, namalizia kwa kuwahakikishia ushirikiano, bunge letu litakuwa pamoja nanyi na kama mtahitaji msaada wetu kwa jambo lolote lile wakati wowote ofisi ziko wazi.”

Katika hatua nyingine, Spika Ndugai amewapongeza viongozi walioapishwa leo na kuwapa pole kutokana na kasi ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano huku akiwataka kufanya kazi kwa bidii ili kuendana na kasi hiyo.

Akijibu maombi ya Spika Ndugai, Rais Magufuli amesema mawaziri hawana likizo kwa kuwa wananchi wanaowaongoza hawana likizo, na kuwataka kukubali kuteseka katika kipindi hiki cha miaka mitano ya awamu ya kwanza ya uongozi wake ili kuwaletea maendeleo watanzania.

“Kwa makatibu wakuu na wizara, najua mna majukumu makubwa ndio maana mheshimiwa spika anazungumza hamjachukua likizo lakini na mimi sijachukua likizo, wananchi unaowaongoza hawana likizo watanzania hawa wote milioni 55 hawana likizo katika shughuli zao kwa hiyo wakati mwingine inakuwa vigumu kuchukua likizo sababu tunaowaongoza hawana likizo,” amesema na kuongeza Rais Magufuli.

“Leo sijalala nilikuwa nazungumza na waliokwenda kuchukua ndege ya ‘Air Bus’, kujua kama wamechukua spea na kui ‘test’ ndege (kuijaribu ndege), wakaniambia tumekaa angani masaa manne ndege inazunguka, kwa hiyo tukichukua likizo, angalau hii miaka mitano tuteseke kuwatumikia watanzania.”

Via>> Mwanahalisi online

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527