Picha : MAKAMU WA RAIS BUNGE LA AFRIKA AWAPONGEZA WALIOSHIRIKI MICHUANO YA UVCCM CUP SHINYANGA

Chama cha mapinduzi CCM kata ya Kambarage Mjini Shinyanga kimefanya sherehe ya kuzipongeza timu za vijana za mpira wa miguu zilizoshiriki katika mashindano ya ya Kombe la Vijana (UVCCM CUP) wilaya ya Shinyanga.

Sherehe hiyo imefanyika Jumanne , Januari 1, 2019 katika ukumbi wa Shy Villa uliopo Kambarage Mjini Shinyanga ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika ambaye pia Mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini Mh.Stephen Masele. 

Akizungumza wakati wa sherehe hizo, Mh. Masele aliwapongeza vijana walioshiriki katika michuano ya Kombe la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) huku akiwataka kuongeza bidii zaidi katika soka ili waweze kuonekana na vilabu vikubwa . 

"Endeleeni kushirikiana maana mpira wa miguu ni kama siasa ni kazi ya kitimu kwenye siasa huwezi fanikiwa peke yako lazima uende na wenzako, kwa hiyo mkijitahidi hata timu yetu ya stand lazima iweke jicho lake kuangalia wachezaji wa nyumbani",alisema Masele. 

Katika hatua nyingine Mh. Masele aliwakumbusha UVCCM kupuuzia maneno ya watu yenye lengo la kuwakatisha tamaa na badala yake waongeze ushirikaiano zaidi katika kufanya kazi. 

"Msiwe na wasiwasi maneno haya yapo tu siku zote kwa hiyo fanyeni kazi simamie misingi ya chama , ukisikia maneno na ukaendelea kufanya kazi ndiyo kukomaa huko", alisema Masele. 

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kambarage Hassan Mwendapole alisema lengo la kufanya sherehe hiyo ni kuwakutanisha vijana wote walioshiriki katika mashindano hayo ili kujenga umoja na mshikamano ambao utakuwa chachu ya maendeleo katika wilaya ya Shinyanga. 

"Haya mashindano yamechezwa karibu wiki tatu , kila siku vijana walikuwa wanakutana kwa hiyo unakuwa umewaweka pamoja hata muda wa kutembea hovyo haukuwepo", alisema Mwendapole. 

Mashindano ya kombe la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM CUP) yalijumuisha kata zote za wilaya ya Shinyanga na aliyeibuka kidedea ni timu ya kata ya Kambarage na kukabidhiwa ngao, cheti pamoja na ng’ombe.

Angalia picha za matukio hapa chini

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Abubakary Mukadam (kushoto) akiteta jambo na Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika ambaye pia Mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini Mh.Stephen Masele wakati wa sherehe ya kuzipongeza timu za vijana za mpira wa miguu, zilizoshiriki katika mashindano ya ya Kombe la Vijana (UVCCM CUP) wilaya ya ShinyangaPicha zote na Steve Kanyefu- Malunde1 blog


Diwani wa Kata ya Kambarage Hassan Mwendapole akisisitiza jambo wakati wa sherehe hizo ambapo amewataka vijana kuendeleza ushirikiano katika michezo ili kuwa chachu ya mendeleo. 


Mwenyekiti wa mashindano ya kombe la Vijana UVCCM, Bi. Jackline Chacha akizungumza wakati wa sherehe ya kuzipongeza timu za vijana za mpira wa miguu, zilizoshiriki katika mashindano ya Kombe la Vijana wa CCM(UVCCM CUP) wilaya ya Shinyanga. Alisema lengo la mashindano hayo ni kutekeleza ilani ya CCM ,huku akiweka wazi kuwa wameunda timu ya wilaya itakayowahusisha vijana kutoka katika timu zilizoshiriki.


Katibu wa UVCCM wilaya ya Shinyanga Comrade Hussein Egobano akisisitiza jambo katika sherehe hiyo.

Andrew Manyonyi Kampteni  wa timu ya Kata ya Kambarage akiwaomba wadau wa soka mkoani Shinyanga  kujitokeza kusaidia timu za vijana kwani wanakumbana na changamoto mbalimbali hasa upande wa vifaa vya michezo.
Mbunge wa Shinyanga Mjini Mh. Masele akipokea hati ya pongezi kutokana na mchango wake ndani ya Chama CCM wilaya ya Shinyanga.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Geofrey Mwangulumbi akipokea hati ya pongezi kutoka kwa mgeni rasmi Mh. Masele.
Mh. Stephen Masele akimkabidhi Comrade Hussein Egobano (kushoto) cheti cha pongezi kutokana na mchango wake kwa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) wilaya ya Shinyanga.
Mh.Stephen  Masele akikata keki katika sherehe hiyo, kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Abubakary Mukadam na kushoto ni Mwenyekiti CCM kata ya Kambarage Rehema Nhamanilo.

Baadhi ya wachezaji wa Timu ya Kambarage wakiwa eneo la Sherehe wakifuatilia yaliyokuwa yanayojiri.
Wadau  wa michezo pamoja na wanachama wa CCM wakifuatilia kwa makini kilichokuwa kinaendelea katika sherehe hizo.
Sherehe inaendelea
Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika  na Mbunge wa Shinyanga Mjini Stephen Masele akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa michuano ya UVCCM CUP Wilaya ya Shinyanga timu kutoka Kata ya Kambarage Mjini Shinyanga.

Picha na Steve Kanyefu- Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527