Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Dk Halfany Haule amewataka watumishi na wenye viti wa serikali za mitaa Manispaa ya Sumbawanga, wajiepushe na visa vya kuomba rushwa wanapopitisha barua za wajasiriamali, wanaoomba vitambulisho maalumu vilivyotolewa na Rais John Magufuli.
Aidha, amewataka wajasiriamali wadogo wakiwemo machinga waliopewa na watakaopewa vitambulisho hivyo maalumu, wasivitumie kama tiketi ya kuvunja sheria na kukiuka maelekezo ya serikali.
Hayo yamebainishwa na Dk Haule wakati wa kuwagawia wajasiriamali wadogo wa manispaa hiyo vitambulisho maalumu.
Alisema miongoni mwa watakaopewa ni machinga na waganga wa tiba asili waliosajiliwa. Wilaya ya Sumbawanga kiutawala ina halmashauri mbili za wilaya ya Sumbawanga na manispaa ya Sumbawanga, ambapo kila moja imepewa vitambulisho 6,250.
“Wenyeviti wa serikali za mitaa msijihusishe kuomba rushwa ili kupitisha barua za wajasiriamali wadogo za utambulisho ambao wana sifa ya kupewa... wanapofika kwenye ofisi hizo wasiombwe rushwa na wapitishiwe barua zao za utambulisho bila kutoa hata senti tano watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kinidhamu na kihalifu,” alionya.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Jacob Mtalitinya alitaja sifa za wajasiriamali ambao watapewa vitambulisho hivyo kuwa ni kuwa na mtaji wa biashara usiozidi Sh milioni nne, wasiwe wamesajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na pia watalipa Sh 20,000, ikiwa ni gharama ya kitambulisho.
“Niwahakikishie kila mwananchi mwenye sifa atapata kitambulisho... nawaasa wawe waaminifu katika kutoa taarifa zao waepuke kudanganya kwa kuwa ni kosa pia,” alibainisha.
Aliwataka wajasiriamali wadogo watakaopewa vitambulisho hivyo, wahakikishe wanavivaa ili wasibughudhiwe.
Petro Makasa ambaye ni baba lishe aliyepatiwa kitambulisho chake, alimshukuru Rais Magufuli kwa nia yake njema kufanya jambo hilo kubwa huku akisisitiza azidi kubarikiwa.
“Niwaombe wajasiriamali wadogo wenye sifa wasipoteze nafasi hii wala wasipuuzie wajitokeze kwa wingi kuviomba,” alieleza Makasa.
Christina Mtawa anayemiliki saluni ya kike alisema, “Hatua hii ya serikali ya awamu ya tano ni ya kupongezwa sana hakika sasa tutapumzika na usumbufu wa maofisa wa TRA,” alisema Makasa.
Peti Siyame, Sumbawanga
Chanzo - Habarileo