BINTI ASIMULIA ALIVYOISHI MWANAE ALIVYOISHI KABATINI...


Licha ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto kudai kwamba madai ya mtoto wa miezi mitano kufungiwa kabatini sio ya kweli, mama mzazi wa kichanga hicho amesimulia jinsi alivyotumia mbinu kuokoa maisha ya mwanaye kabatini.

Katika tukio hilo ambalo linafanana na lile la mwaka 2014 la Mariamu Said wa Morogoro kumficha mtoto wa marehemu mdogo wake kwenye boksi kwa miaka minne, mama wa mtoto huyo amedai kuwa alikuwa akitakiwa kufanya hivyo na mwajiri wake ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi jijini Dodoma.

Akizungumza na Mwananchi jana, mzazi huyo mwenye umri wa miaka 15 alisimulia jinsi alivyolazimika kuvunja sehemu ya nyuma ya kabati ili mwanaye aweze kupata hewa bila mwajiri wake kujua.

Binti huyo na mwanaye ambao wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Dodoma alisema alivunja mbao katika kabati hilo ili mwanaye apate hewa, wakati mwingine alikuwa akitumia upenyo huo kumnyonyesha kwa siri anapokuwa mwenyewe nyumbani hasa mchana.

“Hakujua kama nilivunja mbao nyepesi nyuma ya kabati lake lakini angejua sijui ingekuwaje maana asingekubali kilichofanyika,” alisema.

Binti huyo alidai kuwa ameishi kwa mwajiri wake zaidi ya mwaka mmoja na nusu baada ya kumchukua kutoka Kijiji cha Kigwe, Bahi. 

“Ila tangu aliponichukua hakuwahi kunilipa mshahara, alikuwa akinipa chakula tu,” alidai. “Mwanzoni aliniambia atakuwa akinilipa Sh30,000 kwa mwezi lakini sijawahi kupewa hata mia. Nilipata ujauzito nikiwa kwake na aliyenipa ni (anamtaja jina), ila tangu nimejifungua huyu mama amekuwa akinipiga.


“Asiponipiga yeye basi nitapigwa na mtoto wake wa kiume. Huyu mtoto wangu sijawahi kumnyonyesha mchana. Alikuwa akimuweka kwenye kabati lake la nguo lakini ikifika saa nane usiku ndipo ananipa nimnyonyeshe halafu asubuhi anamchukua tena.”

Polisi wakana kabati

Wakati mzazi huyo akisema hayo, Kamanda Muroto alisema wanamshikilia mwalimu huyo lakini amekanusha kukifungia kichanga hicho kabatini.


Na Habel Chidawali na Rachel Chibwete mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527