SUMAYE : MUSWADA WA SIASA UKIACHIWA UTATAFUNA MPAKA CCM


Baraza Kuu la Chadema Kanda ya Pwani limetaka serikali kuuondoa muswada wa vyama vya siasa uliowasilishwa bungeni, kwa sababu unakiuka katiba kwa kuwa baadhi ya vifungu vyake vinaua demokrasia ya vyama vingi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa kanda hiyo, Frederick Sumaye amesema endapo wabunge hususan wa CCM wakiupitisha muswada huo, itakuwa ndio mwisho wa demokrasia, na kuwataka wabunge kuupinga kwa kuwa moto wake hautaunguza wapinzani pekee, bali hata wao utawaunguza.

Sumaye ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu, amewatahadharisha wabunge wa CCM kwamba endapo muswada huo wataupitisha demokrasia itakufa hadi ndani ya chama chao kwa kuwa mtu mmoja ndiye atakuwa na mamlaka ya kuamua wagombea wa ubunge na hata urais.

“Nawatahadharisha wabunge kama muswada huo utapita demokrasia itakufa hata ndani ya CCM mtu mmoja atakuwa na mamlaka ya kuamua nani awe mbunge au Rais,” amesema Sumaye.

Katika hatua nyingine, Sumaye amesema pamoja na mazingira magumu ya demokrasia, wataendelea kufanya siasa.

“Tunachotaka CCM itoke madarakani kupitia sanduku la kura ili tuwe na nchi ya upendo kama yalivyo mataifa mengine, hatuna haja ya kwenda ulaya ,” amesema na kuongeza.

“Na naamini Watanzania ni waelewa, kila mmoja ananung’unika kivyake sasa hawa wote naamini hawezi kuona mambo haya yanaendelea wananyamaza tu, itafikia hatua watasema hapana, naamini serikali ni sikivu haya tunayoandika wanasikia na watachukua hatua ili tusije fika huko tunakotaka kutoka.”

Sumaye ameeleza kuwa“Katika mfumo wa demokrasia wa vyama vingi, hakuna serikali isiyosemwa na wananchi wake sababu ndio walioiweka madarakani. Lengo kuu la demokrasia ya vyama vingi ni kutoa uhuru kwa wananchi kutoa maoni yao hata kama wanapinga maoni ya kiongozi.

Maoni ya tofauti ni kioo chako katika utawala ili uonyeshwe yale ambayo wa upande wako hawatakuambia au kukuonyesha, mfumo ambao haukubali kukosolewa kwa kiongozi wake au serikali yake ni mfumo wa utawala wa kiimla au wa kidikteta,” amesema na kuongeza Sumaye.

Chanzo - Mwanahalisi online

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post