MAALIM SEIF AKUBALI YAISHE KWA LIPUMBA


Pichani Mwenyekiti wa CUF anayetambulika na msajili, Prof. Ibrahim Lipumba (kulia) akiwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha hicho Maalim Seif Sharif Hamadi.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamadi anatarajiwa kushiriki kampeni za kumnadi Mgombea Ubunge jimbo la Liwale Mohammed Mtesa ambaye amepitishwa na Mwenyekiti wa chama na anayetambuliwa na Msajili wa Vyama nchini Profesa Ibrahim Lipumba.

na wawili wao huenda wakapanda jukwaa moja kumnadi mgombea wao wa ubunge katika jimbo la Liwale.

Akizungumza na www.eatv.tv Mwenyekiti wa Wabunge wa (CUF) Mkoa wa Lindi (Mbunge wa Kilwa Kusini) Selemani Bungara “Bwege” anayemuunga mkono Maalim Seif amesema pande hizo zimeamua kuweka pembeni tofauti zao badala yake watamuunga mkono mgombea aliyesimamishwa na Chama hicho, licha ya kupitishwa na Profesa Lipumba.

“Ni jambo jema Kwetu, tumeamua kuweka tofauti zetu pembeni, mimi nafanya kampeni japo simkubali Profesa Lipumba, huwezi kusema Nguruwe haramu halafu mchuzi wake si haramu kwa hiyo msimamo wetu tumeamua kuweka tofauti zetu pembeni kumuunga mkono Mgombea wetu.”, amesema Bwege.

Awali www.eatv.tv imezungumza Naibu Mkurugenzi wa Habari CUF anayemuunga mkono Maalim Seif Mbarara Maharagande amesema kiongozi wao atafunga Kampeni jimbo la Liwale kuelekea uchaguzi utakaofanyika mwezi huu baada ya aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo kuhamia CCM.

“Sisi upande wetu hatuna tatizo, kwa sababu yule ni mwenyekiti wetu wa halmashauri na viongozi wetu wameshaelekea huko kumuunga mkono, na Maalim Seif wiki hii anatarajia kwenda kufunga kampeni, Sisi ndio tulimwambia akachukue fomu na apitishe kwa upande wa Lipumba kwa sababu ndie anayetambuliwa na dola.”, amesema Maharagande.

Hivi karibuni akinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Kaimu Katibu Mkuu wa CUF anayemuunga mkono Profesa Lipumba Magdalena Sakaya alionesha hofu kwa ya Maalim Seif kushiriki kampeni za mgombea waliompitisha wao kwa kile alichokidai inalenga kuihujumu CUF.

www.eatv.tv ilijaribu kumtafuta Profesa Lipumba lakini hakupokea simu na kupitia afisa habari wake Abdallah Kambaya alisema atafutwe badae kuzungumzia suala hilo. Mgogoro uongozi baina ya pande izo mbili bado upo mahakamani.
Chanzo-EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527