WANANDOA MATATANI KWA TUHUMA YA KUUA BINTI YAO


 
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba linawashikilia baba na mama wa familia moja wakazi wa shehia ya Kiungoni wilaya ya Wete kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wao wa kike mwenye umri wa miezi minane, Rahila Abdalla Othman.


Wazazi hao Abdalla Othman Said na Amina Juma Khatib hadi sasa wanaendelea kuhojiwa na Polisi baada ya mtoto wao kukutwa kisimani akiwa amefariki dunia katika tukio lililotokea Septemba 28, 2018 majira ya saa tatu asubuhi.


Akizungumza na MCL Digital leo Oktoba 1, 2018, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Sheikhan Mohamed Sheikhan amesema licha ya kuwashikilia wanandoa hao pia jeshi hilo linawashikilia vijana wengine ambao waliachiwa jukumu la ulezi kwa mtoto huyo wakati wazazi wake walipokwenda harusini.


Sheikhan amesema kwa mujibu wa maelezo waliyopokea kutoka kwa wataalamu wa afya, mtoto huyo inaonyesha alifariki dunia kabla ya kuingia kwenye kisima hicho ambapo maiti yake ilipatikana.


Amesema kutokana na maelezo hayo wamepata mashaka juu ya kifo cha mtoto huyo ukizingatia umbali uliopo kutoka kwenye makazi ya mtoto huyo na umri wake hadi kwenye kisima alichokutwa mtoto huyo akiwa ameshafariki.


“Mtoto huyu ana umri wa miezi minane tu na maiti yake imekwenda kukutwa ndani ya kisima ikiwa inaelea ukizingatia kisima hicho pia kipo mbali, hapa bila shaka kuna jambo na lazima tufanye upelelezi wa hali ya juu kugundua taarifa zaidi kuhusu tukio hili’’ amesema Sheikhan.

 Chanzo-Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post