Rangi na kope bandia za macho.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kupitia kwa Kaimu Meneja wa Mpango wa Huduma za Macho, Dkt. Bernadetha Shilio, imeeleza kuwa ongezeko la watu wenye matatizo ya macho nchini ni kutokana na matumizi ya vitu vingi, vikiwemo rangi na kope za bandia.
Dkt. Shilio amebainisha hilo leo jijini Dodoma kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya afya ya macho duniani, ambapo ameweka wazi kuwa watanzania wengi wanakabiliwa na tatizo la macho kwa kutofuata masharti ya afya ya macho.
''Rangi za kupaka kwenye ukingo wa macho, kope bandia, kuvaa miwani bila kupima, kutumia dawa za mgonjwa wa macho bila ushauri wa daktari pamoja na kutokula vyakula bora vyenye virutubisho ni chanzo kikubwa cha kuathiri afya ya macho'', amesema.
Aidha mtaalamu huyo wa macho nchini ameongeza kuwa binadamu anatakiwa kujiwekea utaratibu wa kupima macho angalau mara moja kwa mwaka ili kusaidia kutatau tatizo hilo likiwa dogo au kupata usharui wa jinsi gani ya kutunza macho yake.
Asilimia 50 ya wagonjwa wote wanaofika katika hospitali ya Sinza Palestina katika manispaa ya Ubungo jijini Dar es salaam na kupima magonjwa mbali mbali yakiwemo ya Kisukari na Moyo, wanagundulika kuwa na matatizo ya macho ikiwemo muono hafifu.
Katika hospitali ya Sinza Palestina, Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Amina Mnanjota amesema asilimia 50 ya wagonjwa wote wanaofika hospitalini hapo wanagundulika kuwa na matatizo ya macho likiwemo tatizo hilo la muono hafifu.