Na Mwandishi wetu,Dodoma
Watumishi wa Wizara ya Madini na taasisi zake wametakiwa kuzingatia kwa vitendo viwango vya Kijamii, Mazingira na Utawala Bora (ESG) katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, ili kuimarisha uwajibikaji, uendelevu na utawala bora katika sekta ya madini nchini.
Wito huo umetolewa leo Februari 27, 2026 jijini Dodoma na Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga, wakati akifunga mafunzo maalum yaliyolenga kuwajengea uwezo watumishi kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira, kuheshimu masuala ya kijamii na kuzingatia misingi ya uwazi na maadili katika utendaji kazi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mwanga amesema utekelezaji madhubuti wa kanuni za ESG utachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza imani ya wawekezaji, kulinda maslahi ya jamii zinazozunguka maeneo ya migodi pamoja na kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amefafanua kuwa kwa sasa masuala ya utunzaji wa mazingira, matumizi ya nishati safi, kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa, usalama kazini na uwazi wa taarifa za kifedha ni miongoni mwa vigezo muhimu vinavyozingatiwa na wawekezaji kabla ya kuwekeza katika sekta ya madini. Hivyo, mafunzo hayo yamewapa watumishi uelewa mpana kuhusu umuhimu wa tathmini za athari za mazingira, ushirikishwaji wa wadau pamoja na kuzingatia misingi ya maadili na uwajibikaji katika maamuzi ya kiutendaji.
Dkt. Mwanga ameongeza kuwa kuzingatia viwango vya ESG ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuiwezesha sekta ya madini kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa kwa njia endelevu inayokubalika kimataifa.
Akizungumza kwa niaba ya waandaaji wa mafunzo hayo, Mratibu wa Mafunzo ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini, CPA Pili Kamali, amesema moja ya malengo makuu ya mafunzo ni kuhakikisha watumishi wanaandaa na kuwasilisha taarifa za fedha kwa kuzingatia misingi ya ESG, hatua itakayoongeza uwazi, uwajibikaji na uaminifu katika usimamizi wa rasilimali za madini.
Kamali amefafanua kuwa uandaaji wa taarifa za fedha unaozingatia ESG hujumuisha tathmini ya athari za mazingira, kijamii na kiutawala, kwa kufuata maelekezo na viwango vinavyotolewa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi (NBAA).
Kwa ujumla, mafunzo hayo yameelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha uwajibikaji wa taasisi za umma na kuhakikisha sekta ya madini inaendeshwa kwa misingi ya uendelevu, uwazi na manufaa mapana kwa taifa.



Social Plugin