Sunday, August 5, 2018

WAZIRI MKUU AMJULIA HALI WAZIRI KIGWANGALLA NA MZEE MAJUTO MUHIMBILI

  Malunde       Sunday, August 5, 2018
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Mkewe Mary wakimpa pole Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es salaam Agosti 5, 2018, akipewa matibabu baada ya kupata ajali.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es salaam akipatiwa matibabu baada ya kupata ajali Agosti 5, 2018,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Mkewe Mary wakimpa pole Msanii Amri Athumani (Mzee Majuto), ambaye amelazwa katika hospitali ya Muhimbili, jijini Dar es salaam Agosti 4, 2018, kushoto ni Mke wa Mzee Majuto, Aisha Mbwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimjulia hali mama wa Mthamini Mkuu wa Serikali, Evelyne Mugasha wa kwanza kulia, ambaye amelazwa katika Taasisi ya Jakaya Kikwete, Muhimbili jijini Dar es salaam Agosti 4, 2018, kutoka kushoto ni Dk. Tulizo Sanga, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, -Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtembelea na kumpa pole Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) akipatiwa matibabu baada ya kupata ajali.

Akiwa hospitalini hapo leo (Jumapili, Agosti 5, 2018), Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa amesema amefarijika baada ya kumkuta Dkt. Kigwangalla na wagonjwa wengine waliolazwa katika hospitali hiyo wakihudumiwa vizuri.


“Hospitali ya Muhimbili ndio kimbilio letu kwa sasa na tunawashukuru madaktari na wauguzi kwa kazi nzuri mnayoifanya ambayo inaliletea heshima Taifa letu kwani hata watu wa Comoro wanakuja kutibiwa Muhimbili,” amesema.


Kwa upande wakeDkt. Kigwangalla amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu ajali ilikuwa mbaya sana. “Ajali ilikuwa mbaya sana hivi sasa naongea hapa namshukuru Mungu, Serikali pamoja na madaktari na wauguzi kwa jitihada kubwa walizozifanya,”.


Dkt. Kigwangalla alipata ajali jana asubuhi (Jumamosi, Agosti 4, 2018) katikati ya vijiji vya Mdolii na Minjingu wilaya ya Babati mkoani Manyara baada ya gari lake kupinduka na kusababisha kifo cha Afisa Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Hamza Temba na wengine watano akiwemo Dkt. Kigwangalla kujeruhiwa.


Pia Waziri Mkuu amjulia hali msanii maarufu wa maigizo nchini, Bw. Amri Athumani maarufu King Majuto ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akipatiwa matibabu. Amesema amefarijika kumkuta akiwa anaendelea vizuri.


Naye Mzee Majuto amesema anaishukuru Serikali kwa sababu inamuhudumia vizuri. “Mheshimiwa nakushukuru sana na naishukuru Serikali kwani hata sijui ingekuwaje kama si msaada wa Serikali. Hii ni bahati kubwa,”.


Pia Waziri Mkuu amemjulia hali Bibi Hellena Baruti ambaye ni mama mzazi wa Mthamini Mkuu wa Serikali Bibi Evelyne Mugasha aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) akipatiwa matibabu.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, AGOSTI 5, 2018.
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post