AJALI YA BASI NA LORI YAUA WANAFUNZI 9,KUJERUHI 32

Wanafunzi tisa wa Shule ya msingi ya St. Gabriel huko Mwingi, Kaunti ya Kitui nchini Kenya, wamefariki huku wengine 32 wakiwa wamejeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi ya shule na lori usiku wa Jumamosi kuamkia leo.


Wanafunzi nane wametajwa kufariki katika eneo la ajali hiyo huku mmoja ambaye anaongeza idadi ya kufika tisa amefariki akiwa hospitali ya taifa wakati anapatiwa matibabu.


Wanafunzi hao walikuwa wakitokea Mombasa kwenda katika safari ya kimasomo ambapo basi lao liligongana uso kwa uso na Lori katika daraja la Kanginga, Kilomita moja kutoka mji wa Mwingi kwenye barabara ya Thika-Garissa usiku wa manane.


Aidha kati ya majeruhi 32 ya wanafunzi ya waliofikishwa katika Hospitali ya Mwingi, wanafunzi Sita wanadaiwa kuwa katika hali mbaya (mmoja amefariki na kubaki watano) ambapo wameshahamishwa katika hospitali ya Taifa ya Kenya, (Kenyatta National Hospital).


Wanafunzi nane waliofariki ni kati ya abiria 50 waliokuwa kwenye basi hilo pamoja na walimu.


Katika ujumbe wake kwa wazazi na walezi wa wanafunzi, Rais Kenyatta amesema ni bahati mbaya kwamba maisha ya wanafunzi wasio na hatia yamekatisshwa na kwamba "Tumewapoteza wale ambao tulitegemea kujenga nao taifa siku za usoni".


Aidha Dereva wa lori hilo tayari amekwishakamatwa na Jumatatu atafikishwa mahakamani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527