Friday, August 31, 2018

GARI LA WAGONJWA LA JWTZ LAUA NA KUJERUHI WATU WANNE CHALINZE

  Malunde       Friday, August 31, 2018
Kamanda wa Polisi Pwani Wankyo Nyigesa akitoa taarifa ya ajali ya gari la wagonjwa mali ya jeshi la wananchi JWTZ inayoonekana pichani iliyogonga gari jingine eneo la Kibiki Chalinze.

Na Julieth Ngarabali, Mwananchi

 Mtu mmoja amefariki dunia na wanne kujeruhiwa baada ya gari la kubeba wagonjwa la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuligonga gari jingine kwa nyuma katika eneo la Kibiki kata ya Bwilingu halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani.

Akizungumza leo Ijumaa Agosti 31, 2018 Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Wankyo Nyigesa amesema ajali hiyo imetokea leo ikihusisha gari hilo la wagonjwa la kikosi cha 911KJ cha Ihumwa, Dodoma.

Amesema gari hilo lilikuwa linasafirisha mgonjwa kutoka mkoani Dodoma kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam.

Amemtaja aliyefariki dunia kuwa ni Elinikunda Mushi (50) ambaye alikuwa mgonjwa, kwamba alikuwa amekwenda Ihumwa kwa mwanae, Ufo Swai.

“Hili gari la JWTZ lilikua linaendeshwa na askari Shabani Mpwate, lilipofika eneo la Kibiki dereva aliligonga gari jingine aina ya Toyota Canter kwa nyuma, Canter hilo lilikuwa limeegeshwa kando ya barabara kwa matengenezo,” amesema.

Amewataja majeruhi katika ajali hiyo kuwa ni Beatrice Shidodolo ambaye ni muuguzi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, dereva wa gari lililogongwa, Justine Patrick na fundi wa gari hilo, Rashid Rais pamoja na Swai.

Amesema katika uchunguzi wa awali wamebaini kuwa katika gari hilo la wagonjwa pia kulikuwa na watu wengine wanne ambao hawakupata majeraha yoyote.

Amesema abiria hao ni askari MT 3480 SGT Elimasa Mushi, MT 95881 PTE Taulin Karia, Eveline Stanley (25) na mtoto mwenye umri wa miezi 11, Nicholous Petro.

Amebainisha kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam huku majeruhi pia wakipata matibabu katika hospitali hiyo.

“Dereva wa gari la JWTZ tunamshikilia kwa mahojiano na uchunguzi kwa sababu hata kama ni gari la wagonjwa lazima tujiridhishe na sisi,” amesema.

Chanzo - Mwananchi
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post