KATIBU MKUU WA CCM AWACHIMBA MKWARA VIJANA WA CCM MIJADALA MITANDAONI

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema chama hicho kinafuatilia majadiliano ya wanachama wao katika mitandao ya kijamii ili kujiridhisha kuwa haivuki mipaka ya uhuru wao.


Akizungumza leo Ijumaa Agosti 31, 2018 katika ufunguzi wa baraza kuu la vijana wa chama hicho (UVCCM) amesema mitandao hiyo imekuwa chanzo cha fitna, kebehi na kuchafuana.


Amesema wakati mwingine mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli anachafuliwa katika mitandao hiyo na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa na UVCCM kulinda hadhi ya taasisi ya urais na chama.


“Tunafuatilia mijadala ya wanachama wetu wote ndani ya chama na jumuia ili tujiridhishe hawavuki mipaka ya uhuru wa kujadili masuala ya chama ndani ya mitandao hiyo,” amesema.


Ametoa mfano wa kiongozi mmoja (bila kumtaja jina) wa UVCCM mkoani Mara kuwa alikuwa akiingilia masuala ya kisheria na kuandika mambo ya ovyo mitandaoni kuhusu Serikali.


Amesema mambo aliyokuwa akiandika kiongozi huyo hayakuwa na ukweli na hivyo kusababisha taharuki.


“Pamoja na ujana wenu katiba zetu na kanuni hazina eneo ambalo limeandikwa mikutano na vikao katika mitandao ya jamii. Mnapoteza muda na kujidhalilisha kuanza kujadili mambo ambayo yalitakiwa kujadiliwa kwenye vikao,” amesema.


Amesema wanawategemea vijana kutangaza mambo ya chama lakini wanayotakiwa kuyatangaza ni yale yaliyokwishajadiliwa katika vikao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527