DC NDAGALA AKABIDHI ZAWADI YA MABATI 280 KWA WALIMU WASTAAFU KAKONKO

Mkuu  wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala amekabidhi mabati 280 kwa walimu wastaafu 14 kwa niaba ya kamati tendaji ya Chama cha walimu Wilaya ya Kakonko (CWT)  kama zawadi kwa kufanya kazi iliyotukuka kwa kipindi chote cha utumishi wao.
 
Akikabidhi mabati hayo jana kwa wastaafu katika ofisi za Chama cha waalimu CWT Wilayani Kakonko  Kanali Ndagala aliwapongeza wastaafu hao na kuwasisitiza kutumia zawadi waliyopewa kukamilisha nyumba zao au kuanzisha biashara itakayowasaidia kuendeleza maisha yao.
 
Alisema kila msataafu amegawiwa mabati 20 kama zawadi za pongezi kutokana uadilifu pamoja na kujituma wakati wakiitumikia serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, katika sekta ya elimu ambapo chama hicho kimetambua utendaji wao uliotukuka.
 
“Niwapongeze kwa kumaliza salama muda wenu, mnapoenda kuanza maisha mapya na mazuri, huu ni mwanzo mzuri kama hujamalizia kibanda kamalizie, kama tayari ni vizuri kujenga kibanda cha biashara au kufuga ili kuweza kujikimu kwa kipindi hiki maana kuna maisha baada ya kustaafu”, alisema Kanali Ndagala.
 
Aidha alitoa wito wa kujitoa na kuwaomba watumishi wanapokuwa kazini wajiandae kustaafu kwani kustaafu siyo mwisho wa maisha bali ni mwanzo wa maisha mengine uraiani na kwamba fursa ni nyingi endapo watazitumia vizuri na kuwataka kutokata tamaa kutokana a changamoto zinazojitokeza kazini kwani serikali inatatua changamoto moja hadi nyingine na kuomba ushirikiano udumishwe ndani ya chama cha walimu.
  
Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa Chama cha Walimu wilaya ya Kakonko Tumaini Daniel aliwaomba walimu wastaafu kuwakumbusha walimu waliopo kazini kujituma wakati wa kazi na kuiomba halmashauri itenge bajeti ya kuwarudisha  makwao wastaafu baada ya kustaafu na Halmashauri iwaingize waalimu kwenye bajeti ya 2018/19 ili wapande madaraja kwani kuna waalimu zaidi ya 400 wanaotakiwa kupanda madaraja.
 
Mmoja wa wastaafu Masuhuko Magwaya aliyekuwa akifundisha shule ya msingi Bukiriro alieleza kufurahishwa na zawadi hizo walizopewa na kuwaomba walimu waliopo kazini wafanye kazi kwa uadilifu na kujitoa kwa moyo katika kuhakikisha wanatoa elimu bora kwakuwa Wanafunzi hao ndio tegemeo la kesho.
 
Mninga Lameck mwalimu mstaafu kutoka shule ya msingi Kabingo  amewasisitiza walimu kufanya kazi kwa kujitoa pia watambue kuwa kazi ya ualimu ni wito na kuwataka kutotanguliza taama za kutopenda Malipo kabla ya kazi ili kujjengea heshima na kuweza kustaafu vizuri.
Mkuu  wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akikabidhi mabati - picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Zoezi la makabidhiano likiendelea
Mkuu  wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akizungumza wakati wa kukabidhi mabati kwa walimu wastaafu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527