Magufuli Akutana na Wajumbe wa Sekretarieti ya CCM,Aahidi Kuboresha Maslahi ya Watumishi wa CCM



Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mara ya kwanza amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Sekretarieti ya chama hicho.


Magufuli pia amekutana na wafanyakazi wa CCM Makao Makuu katika Ofisi za Chama hicho Mjini Dodoma ikiwa ni siku tano tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa Tano wa Chama hicho.


Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amekutana na watendaji hao wa CCM kwa lengo la kuwasalimia, kupokea maoni na ushauri wao juu ya utendaji kazi ndani ya Chama.


Katika mazungumzo hayo, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewapongeza watendaji wote wa Chama Cha Mapinduzi kwa kazi kubwa wanayoifanya na kwa namna ya pekee kwa jinsi walivyotoa mchango mkubwa kuhakikisha CCM inapata ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.


Pia amewataka kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa lengo la kuendelea kukiimarisha Chama hicho ambacho kimebeba dhamana ya kuongoza Serikali kwa kipindi kingine cha miaka mitano.


Dkt. Magufuli amewahakikishia kuwa chini ya uongozi wake atafanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa CCM ikiwemo maslahi duni, vitendea kazi na kuondoa utegemezi.


Aidha, Dkt. Magufuli amewataka watumishi wa chama kutoa ushirikiano katika zoezi la uhakiki wa mali za Chama litakalosimamiwa na sekretarieti ya chama na ameahidi kuwa atahakikisha mapato yatokanayo na vyanzo vya mapato vya chama yanatumika ipasavyo.


Kwa upande wao watumishi wa CCM wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Ndugu Abdulrahaman Kinana wamempongeza Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kwa asilimia mia moja na wajumbe wa Mkutano Mkuu uliofanyika tarehe 23 Julai, 2016 Mjini Dodoma kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa.


Watumishi hao wamemuahidi kuendeleza utumishi uliotukuka na wameelezea matumaini yao ya kuboreshewa maslahi.


Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527