Waziri Mkuu :“Kitendo Cha Wbunge Kususia Vikao vya Bunge Hakitoi Picha Nzuri Kwa Wananchi Waliotuchagua"


Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo, Bungeni Mjini Dodoma amewataka wabunge wa upinzani ambao wamesusia vikao vya Bunge tangu Mei 30 kuingia Bungeni na kuacha kususia vikao vya Bunge kwani hakuna tija kwa Taifa.


Mhe. Majaliwa ameyasema hayo alipokuwa akitoa hutuba ya kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la kumi na moja.


“Kitendo cha baadhi ya waheshimiwa wabunge kususia vikao vya Bunge hakitoi picha nzuri kwa wananchi waliotuchagua kuwasilisha matatizo yao katika Bunge hili, hivyo natoa rai kwa waheshimiwa wabunge hao kutafakari upya uamuzi wao na niwasihi kwa busara zao waingie ili kwa pamoja na kwa ushirikiano tuweze kutoa ushauri kwa Serikali,” alisema Mhe. Majaliwa.


Aidha Mhe. Majaliwa alitoa ufafanuzi juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo imetoa haki na kinga kwa waheshimiwa wabunge ili kujadili na kuhoji utendaji wa Serikali kwa uhuru bila mashaka yoyote ya kuweza kushitakiwa wanapotimiza wajibu wao wakiwa Bungeni.


Aliendelea kwa kusema kuwa kinga ya aina hiyo haijatolewa kwa mwananchi yeyote yule Nchini ila kwa Wabunge, hivyo basi hakuna mbunge aliyefungwa mdomo labda aamue kujifunga mdomo yeye mwenyewe.


Mhe. Majaliwa amesema kuwa Bunge linaongozwa na Katiba, Sheria na Kanuni za Kudumu za Bunge, hivyo ni vyema zikafuatwa kuondoa manung’uniko yasiyo ya lazima na endapo kuna utata katika jambo lolote ndani ya Bunge zipo taratibu zilizowekwa na kanuni za kufuata ili kupata ufumbuzi na si kwa kususa kuingia Bungeni kwani hakuna tija kwa Taifa.


Wabunge wa upinzani wamesusia vikao vya Bunge tangu Mei 30, 2016 mpaka leo Juni 30 ambapo Bunge limehitimishwa.


Aidha wabunge hao wamekuwa wakiingia Bungeni kila asubuhi na jioni kisha kutoka mara tu Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson anapomaliza kusoma Dua maalum la kuliombea Bunge na Taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527